Mkoa Wa Dodoma Kuwatambua na Kutatua Changamoto za Wanafunzi Waliochaguliwa Kujiunga Kidato Cha Tano , 2022- Mhe. Mtaka

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe Anthony Mtaka wakati akiongea na vyombo vya habari,kumtambulisha Mwanafunzi Mariam Leonard Mchilo na kuwashukuru wadau mbalimbali ambao wamejitolea kumsaidia mwanafunzi huyo.

Wadau hao ni pamoja na Spika Mstaafu na Mbunge wa Kongwa Mhe.Job Ndugai ambaye  anamhfadhi Mwanafunzi Mariam hadi hapo atakapokamilisha taratibu za kujiunga na kidato cha tano mkatika shule ya sekondari Songea, shule ambayo amepangiwa. Aidha Mhe Mtaka amemshukuru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Maabara ya Taifa Bw. Nyambura Moremi, Mwanza University pamoja na Equity Bank ambao kwa njia moja au nyingine wamechangia ada za masomo na gharama zingine za Mwanafunzi Mariam. 

Akizungumzia Ufadhili wao kwa mwanafunzi Mariam , Makamu Mkuu wa Chuo/ 'Vice Chancellor' wa Mwanza University Prof. Florah Fabian ameeleza kuwa, Mwanza University ni chuo kikuu kipya ambacho kitakuwa kikiendesha elimu ya masomo ya uuguzi na udaktari. Pamoja na elimu hizo kila mwaka  chuo hic hutoa nafasi za kusaidia mwanafunzi mmoja hadi watatu wenye changamoto za kiuchumi na hasa wale ambao wanataka kusoma masomo ya Sayansi ikiwemo elimu ya Uuguzi pamoja na Udaktari."Hivyo baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuhusu Mwanafunzi Maria Mchilo ,uongozi wa chuo umeamua kumsaidia Mariam ada ya shule na kujikimu kwa elimu yake yote ya kidato cha tano,kidato cha Sita pamoja na Chuo kikuu ". Amesema Prof. Fabian.

 Aidha pamoja Na chuo Kikuu Mwanza, Benki ya Equity nayo imeguswa na historia ya Mwanafunzi Mariam na kuamua kumfungulia akaunti ambayo haina gharama kabisa. Akizungumzia akaunti hiyo Meneja wa Tawi la Equity Benki Dodoma Bi. Upendo Makula ameeleza kuwa pamoja na kumfungulia akaunti, benki itamwekea kiasi cha Tsh. 300,000/- ikiwa ni kianzio. Wadau wengine akiwepo Prof. Flora Fabian waliongezea kiasi cha Tsh. 200,000/- na Bw. Nyambura Moremi Tsh. 150,000/- na kufanya akaunti ya mwanafunzi huyo kupokea jumla ya kiasi cha Tsh. 650,000/-.

Mwanafunzi Mariam Leonard Mchilo ni mtoto wa tano katika familia ya watoto 6 wa Bwana na Bibi Mchilo. Elimu yake ya Msingi aliipata katika shule ya msingi Ndachina na elimu ya Sekondari katika shule ya Sekondari Songambele Kilimani, Wilayani Kongwa.Katika mtihani wa kidato cha Nne ambao alifanya mwaka jana 2021, Mariam alipata daraja la kwanza lenye pointi 16 na kuwa Msichana pekee kati ya wanafunzi wanne waliopata daraja la kwanza. Kulingana na mazingira magumu katika familia yake Mariam aliazimia kusoma kwa bidii ili aweze kusaidia familia yake, hali iliyompelekea mara baada ya kumaliza mitihani yake ya kidato cha nne kutafuta kibarua cha mama lishe na hatimae kazi za ndani.Mjomba wake alimsaidia kutafuta kazi za ndani na hatimae 8/5/2022 alifanikiwa kupata kazi jijini Dar Es salaam kwa mama aliyemtaja kwa jina la Agnes Kosamu. "Namshukuru Mama Kosamu kwani yeye ndiye aliyenisaidia kurudisha ndoto yangu kwani baada ya kumueleza kuwa nimemaliza kidato cha nne na kupata division one ya point 16, alininisitiza nirudi shule na kuendelea na Masomo na hivyo akatuma habari zangu kwenye group la WhatsApp na kunichangia Kiasi cha Tsh.180,000/- na kuhakikisha na fika hapa nilipo leo" amesema Mariam. 

Lengo langu nisome hadi chuo kikuu na hatimae nije kuwa muguuzi, nataka kuwa muuguzi kwani baba yangu anakidonda ndugu tangu 1993, kidonda ambacho nadhani amekipata kwa kupasuliwa na kukatwa mshipa fulani wakati wa upasuaji au yeye mwenyewe kwa kutokutii masharti ya madaktari hivyo nataka nikiwa mguuzi niweze kuwasaida watu kama hao. 

Akimwelezea Mwanafunzi Mariam ,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka ameonyesha kufurahishwa na jitihada za mwanafunzi huyo ambaye pamoja na kuishi katika mazingira magumu na kusoma shule ya kutwa ameweza kupata daraja la kwanza lenye point 16, bila shaka kwa kidato cha tano na sita akisoma shule ya bweni anaweza kupata daraja la kwanza la pointi 3. Mhe.Mtaka amewaeleza waandishi hao kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma itahakikisha inampatia Mariam mahitaji yake yote yatakayomwezesha kumaliza kidato cha sita.

 Aidha Mkuu wa Mkoa huyo amewataka Wanafunzi wote wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali hususani wale ambao wamemaliza kidato cha nne katika shule za kata na kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano kuwasiliana na Ofisi za Wakuu wa Wilaya katika maeneo waliyopo na kisha kuwasiliana na Afisa Elimu wa maeneo hayo ili kuelezea changamoto zao na kuona namna bora ya kuwasaidia.

Kushoto Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka akimtambulisha Mwanafunzi Mariam Leonard Mchilo mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza la point 16

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu  Mwanza Prof.Florah Fabian akielezea ufadhili ambao Chuo hicho umeutoa kwa mwanafunzi Mariam

Meneja wa tawi la bank ya Equity Dodoma Bi. Upendo Makula akimpongeza mwanafunzi Mariam na kuahidi kumfungulia akaunti isiyo na g.harama yetote. Benki ya Equity ilimwekea mwanafunzi huyo kiasi cha Tsh.300,000/-

Mkuu wa  Mkoa wa Dodoma Mhe. Mtaka( katikati) akiwa na picha ya pamoja na wafadhili kushoto Prof.Fabian toka Chuo Kikuu Mwanza na Kulia Equity Bank, Wapili kulia Mwanafunzi Mariam

Mwanafunzi Mariam akijaza fomu ya kufungua akauti Equity Bank


Picha ya pamoja ya  Wafadhili wa Mwanafunzi Mariam, wafadhili hao ni  kutoka TBC, Equity Bank na Mwanza University

Mhe. Mtaka akimtaka mwanafunzi Mariam kusoma kwa bidii na kupata daraja la kwanza la point 3.

Mhe. Mtaka ametoa angalizo kwa wazazi kutokutumia wito huo vibaya na kukwepa majukumu yao kwa kujifanya wajane na wagane wa muda na hata yatima wa muda.Mhe. Mtaka amemtaka mwanafunzi Mariam kuwa na moyo wa masomo na kuhakikisha ufaulu wake unaongezeka na kufikia divisheni ya kwanza ya point tatu. Mwisho.

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA