RC MTAKA AKUTANA NA KUFANYA KIKAO NA WAENDESHA BODABODA NA BAJAJI JIJINI DODOMA

 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka, hivi karibuni kwenye ukumbi wa Cavillum jijini Dodoma, alikutana na kuongea na madereva wa Pikipiki maarufu kama Bodaboda pamoja na Bajaji kuzungumzia utendaji kazi wao, hali ya ulinzi na usalama kutokana na matukio ya kihalifu yanayofanywa na baadhi yao pamoja na changamoto wanazokumbana nazo wakati wa usafirishaji wa abiria. 

Katika kikao hicho, Mhe. Mtaka aliongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, wakuu wa idara zinazohusika na usafirishaji kama vile Wakala wa barabara za vijijini TARURA, Mamlaka inayoshughulikia usafirishaji wa nchi kavu LATRA , Mkuu wa kitengo cha Usalama barabarani pamoja na wadau wanaoisaidia kuiwezesha sekta ya usafirishaji kifedha ambao ni Benki ya NMB pamoja na shirika la Bima la SANLAM. 

Baadhi ya madereva wa vyombo hivyo, walitoa malalamiko yao mbele ya Mkuu wa Mkoa kwamba wananyanyaswa na vyombo vinavyohusika na usalama barabarani kwa kulipishwa faini zisizo na risiti, kubabimbikiwa makosa ambayo wakati mwingine hayahusiani na usalama barabarani. 

Akijibu tuhuma hizo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dodoma Bwana Lusako Kilembe, amesema kuwa sheria ya ulipaji faini za barabarani unafanyika kwa kutumia namba maalumu za malipo zinazojulikana kama Control number na si vinginevyo hivyo ametoa wito kwa madereva hao kutokubali kufanya malipo kwa afisa yeyote wa TARURA kwa kumpatia fedha mkononi Pia Bwana Kilembe ameongeza kuwa wapo kwenye mchakato wa kubadilisha mamlaka itakayohusika na upokeaji wa faini za barabarani ambapo Halmashauri ya Jiji ndio itahusika kwa hilo na si TARURA tena. 

Kwa upande wa Mamlaka ya usafirishaji nchi kavu LATRA ambayo pia ilielekezewa malalamiko na madereva hao, Bwana EzekieI Emmanuel, Afisa mfawidhi wa Mamlaka hiyo Dodoma, amejibu baadhi ya tuhuma ikiwemo suala la kukamata pikipiki ikiwa nje ya kituo ambapo alisema vyombo hivyo vinatakiwa kuwa na usajili na kukaa kwenye vituo vyao kusubiri abiria kwani hii itasaidia kupunguza uhalifu. Aidha, ameongeza kuwa, gharama ya kulipia leseni kwa pikipiki kwa mwaka ni shilingi 17,000/-, na kwa bajaji ni shilingi 20,000/- hivyo endapo malipo yatachelewa, huwa kuna faini ya ongezeko la shilingi 10,000/- ambapo amewataka madereva hao kutii sheria bila shuruti na kuzingatia muda wa ulipiaji wa leseni zao ili kuepuka faini hizo. 

RC Mtaka alihitimisha kikao hicho kwa kutoa neno kwa madereva hao kwa kuwaasa kuiheshimu kazi yao na kuitaka Mamlaka husika kuiangalia kwa karibu sheria ya uvaaji wa kofia ngumu kwa abiria wa pikipiki kwani kulingana na hali iliyopo ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19, uchangiaji wa kofia hizo unaweza kuongeza maambukizi zaidi. Amewaasa bodaboda kukerwa na matukio ya uvunjifu wa amani yanayoendelea kufanywa kwa kutumia pikipiki miongoni mwa wenzao wasio waaminifu. Pia amesema lengo la Mkoa ni kutengeneza kundi jipya la wafanyabiashara miongoni mwa pikipiki kwani zitakaposajiliwa itakua rahisi kupata mtandao mkubwa wa abiria na amewataka kuacha mara moja kujichukulia sheria mikononi pindi inapotokea ajali inayohusisha bodaboda. 

Mhe.Mtaka amezisihi mamlaka husika kwa kushirikiana na madereva hao kuhakikisha wanakomesha suala la rushwa na kila dereva ajisajili kwenye mifuko ya penseni kama NSSF, iCHF, NHIF kwani itawapunguzia gharama za matibabu na kupata mafao ya uzeeni pindi atakaposhindwa kuendelea na kazi au kustaafu. Mwisho.

Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe.  Anthony Mtaka akizungumza na Madereva wa  Pikipiki (Bodaboda) na Bajaji na kuwataka kuithamini kazi yao na kutumia kila fursa kujiwekea akiba na hivyo kujihakikishia maisha yao ya sasa na  baadae

Kamishna wa uhamiaji Mkoa wa Dodoma  Bw. Sosthenes Kibwengo,akizungumza na kuwafahamisha madereva wa bodaboda na bajaji kuwa ni haramu kusafirisha abiria haramu na ukikamatwa basi chombo chako kitataifishwa 

Baadhi ya madereva wa Bodaboda na Bajaji wakisikiliza kwa makini mada mbalimbali zikiwasilishwa 

Mwakilishi kutoka Bima ya SANLAM  Bw. Said Makunga akizunguamzia huduma mbalimbali zinazotolewa na bima hiyo kwa waendesha bodaboda na bajaji, ametaja mojawapo wa huuduma yao  inajulikana kama Boda Shua pia wana mifumo ya  teknolojia ya kidijitali.

Meneja benki ya NMB Dodoma akiwakaribisha Madereva wa Bodaboda na bajaji kufungua akaunti katika benki hiyo kwani  NMB ina fursa nyingi

Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Mtaka akisisitiza jambo

Kiongozi wa TARURA akijibu hoja mbali mbalia kama zilivyowakilishwa na madereva wa bodaboda na Bajaji

Kamanda wa Trafiki Mkoa wa Dodoma akijibu na kutoa maelezo kuhusu kero mbalimbla za madereva bajaji na Bodaboda 

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA