“HAKUNA MWANAFUNZI ATAKAYESHINDWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO KWA KUKOSA MICHANGO " RC -MTAKA


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Anthony Mtaka, amekutana na Walimu Wakuu wa shule za sekondari zenye kidato cha Nne na Sita ili kuzungumza nao namna  bora  ya kujiandaa na Elimu bure kwa kidato cha Tano na Sita.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na takribani walimu wakuu 25 wa shule za sekondari za Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ambazo zina  wanafunzi zaidi ya 3,000. Kikao kiliainisha michango inayotozwa na shule.michango ambayo huorodheshwa kwenye fomu ya kujiunga na Kidato cha Tano na ambayo kila mwanafunzi huhitajika  kuwa nayo pindi anapowasili shuleni kwa mara ya kwanza na kusababisha baadhi ya wazazi kushindwa kukidhi mahitaji hayo na kuacha kupeleka watoto wao shule.

Walimu hao walipata nafasi ya kuwasilisha changamoto zitakazowakabili baada ya ondoleo la ada hizo kwani zilikua zikisaidia katika uendeshaji wa shule hasa kulipia ankara za umeme, maji na wasaidizi wa majukumu ya shuleni na kuongeza kuwa mahitaji ya muhimu kama vile Bima ya afya, kuagiza vitendea kazi pamoja na vitabu vya kujisomea ndivyo hasa hupelekea wazazi na walezi kuona kwamba michango ni mingi inayotozwa na shule.

Mhe. Mtaka alisema kuwa Mhe. Rais Samia amefanya maamuzi ya kuondoa ada hizo ili wazazi waweze kupeleka watoto wao shule, bila kikwazo chochote."Elimu bila malipo itawaibua wale walioshindwa kufikika na wasiokua na mwanga wa elimu hivyo lazima tuwalinde Watoto wetu, utamaduni wetu na shule zetu"

Aidha Mkuu wa Mkoa alitoa maagizo kadhaa ikiwa ni pamoja na kila mwanafunzi aliyepangiwa kidato cha Tano  apokelewe kwa mazingira yoyote awe na michango au lah, michango yote inayotozwa na shule isizidi Shilingi 150,00/= kwa mahitaji ya muhimu, mwanafunzi asilazimishwe kununua vitu kwenye duka la shule, wanafunzi wasiwekewe masharti ya aina ya vifaa vya kupeleka shuleni.

Maagizo mengine ni pamoja na kuzitaka Idara za Elimu Mkoa, Halmashauri na Maafisa Elimu kukaa na kupanga mahitaji ya muhimu kwa shule zote na ziwe na kiasi kimoja. Kwa upande wa Bima ya afya, amesema atakaa na DMO kuangalia jinsi ya kuwasaidia wanafunzi watakaohitaji msaada na shule zisubiri mwongozo wa ada kutoka TAMISEMI ambao utatolewa hivi karibuni.

Wito umetolewa na Mhe. Mtaka kwa wazazi na walezi wote kupeleka watoto wote waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na ufafanuzi wa malipo ya ada wataukuta shuleni pia ametaka pasiwepo Mwanafunzi atakayeshindwa kuripoti shuleni kwa kukosa michango iliyopo kwenye fomu ya kujiunga na shule. Aidha Mhe. Mtaka  amewataka walimu kuendelea na moyo mwema wa kuwafundisha watoto kwani kazi yao ni kazi yenye haiba ya pekee na kazi ya Wito.

 MWISHO











 

 


Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA