Kata ya Ipagala Yawapongeza Walimu wa Shule Za Msingi Na Sekondari

 































Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari za Serikali  pamoja na wanafunzi kutoka Kata ya Ipagala, leo wamepongezwa kwenye hafla iliyoandaliwa na Diwani wa Kata hiyo Bw. Gombo Kamuli Doto. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Naibu Waziri- Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Omari Kipanga (Mb) ambapo mwenyeji wake alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Anthony Mtaka.Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtemi Mazengo ambayo ni moja kati ya shule tano za Msingi za mfano nchini Tanzania.

Akielezea Shule hiyo Bw. Gombo amesema kuwa Shule ya Msingi Mtemi Mazengo ni moja kati ya shule 5 za majaribio zilizojengwa na Serikali kwa lengo la kupima ufaulu kulinganisha na ule wa shule binafsi ambapo shule ina Madarasa 17, Miundo mbinu ya umeme na maji, maktaba, nyumba za walimu 4, ukumbi wa mkutano, viti na meza nzuri za kukalia waalimu pamoja na wanafunzi. Ujenzi wa shule hii umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1 ambao kati ya hizo Tsh.700 milioni zilitolewa na Serikali Kuu wakati zilizobakia zilitokana na mapato ya ndani. Shule ya Mteni Mazengo  imehitimisha darasa la Saba la kwanza mwaka 2021 kwa kuwa na wahitimu 84 ambao wote walifaulu kwa viwango vya juu.

Akiendelea, Diwani Gombo alitoa taarifa fupi ya Shule zilizopo katika Kata yake ambapo alieleza kuwa Kata ya Ipagala ina shule Sita za Serikali huku 4 zikiwa shule za msingi na 2 shule za sekondari (shule ya sekondari Makole na shule ya sekondari Meria). Shule za Msingi zina jumla ya wanafunzi 3190 ambao wote wamefanya vizuri kimkoa na Kitaifa katika matokeo ya Mitihani ya Darasa la Nne na darasa la Saba mwaka 2021.

Akizungumza, Mkuu wa Wilaya Mhe. Jabir Shekimweri, alimpongeza Diwani wa Kata hiyo Bw. Gombo na kuwaasa wazazi  kununua wakati ili kupata muda wa kuongea na watoto wao,kwani hiyo itawasaidia Wazazi waweze kufahamu maisha  ya watoto wao wakiwa shule, njiani na hata wanapokua nyumbani kwa kuwa matukio ya ulawiti kwa watoto yameshamiri sana kipindi hiki. Aidha Mhe.Shekimweri amefurahia maendeleo ya shule hiyo na kuahidi kuupeleka Mwenge wa uhuru katika shule hiyo mara utakapo tembelea Mko wa Dodoma. "Nichukue fursa hii kuwafahamisha kuwa hiki ni deni kwangu Mwenge utakapokuja MNkoa wa Dodoma basi nitahakikisha utatenmbelea shule ya Msingi Mtemi Mazengo".Amesema Mhe. Shekimweri. 

Nae, Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde, amempongeza sana Diwani Gombo, kwa kuwathamini na kuwatambua waalimu,kwani hiyo imekuwa chachu katika utendaji kazi wao, pia imewafanya wanafunzi kuzingatia masomo na kufaulu kiasi cha kutoa mwanafunzi wa kwanza katika mashindano yaliyohusisha shule binanfsi.Aidha Mhe. Mavunde amepongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Mtaka kwa kipaumbele chake katika Masuala ya Elimu.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mhe. Anthony Mtaka, ametoa maelekezo kwa shule zote za Serikali Mkoani Dodoma na kuziagiza kuandaa vikao vya wazazi kila muhula, pindi shule zinapofungwa ili kujadili maendeleo ya Elimu kwa watoto wao kwa kuwa malezi ya watoto ni baina ya mzazi, mwalimu na mtoto mwenyewe, kwani matokeo yakiwa mazuri, pongezi huenda kwa wote hivyo wazazi wawajibike kwa watoto wao.

Nae,Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Omary Kipanga,ameeleza kuwa suala la elimu ni la lazima na si hiyari ndio maana Serikali inatimiza wajibu wa kutengeneza Miundombinu Bora ya kufundishia  kwani Taifa Bora ni lile lenye watu wenye elimu." Serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu kwenye Mkoa wa Dodoma ambao ndio makao makuu ya nchi, imetoa Shilingi Bilioni 17 kwa ajili ya Ujenzi wa Chuo kikubwa cha Tehama katika eneo la Nala ambacho tayari kimeanza kujengwa" Mhe. Kipanga

Kwa niaba ya Walimu, Afisa elimu Wilaya ya Dodoma Bi. Celina Shirati alimshukuru Diwani Gombo kwa kuandaa shughuli hiyo na alisema walimu wamejisikia kuheshimiwa, kuthaminiwa na kupendwa hivyo wataendelea kuchapa kazi kwani kipaumbele cha Mkoa ni kusimamia Elimu.

 

MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA