Wajasiliamali Wapewa Mafunzo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma imetoa Mafunzo kwa wajasiriamali wadogo ambao wamewezeshwa mitaji ya biashara na Ofisi hiyo ambapo takribani wajasiriamali 20 walishiriki mafunzo hayo ambayo yalifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Wawezeshaji wa Mafunzo hayo walikuwa wataalamu kutoka Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Dodoma.SIDO ina lengo la kuwasaidia wajasiriamali hao kufungua au kufanya biashara zenye tija.
Akielezea namna ya kufanya biashara yenye tija, Bw. Stephano Ndunguru ambaye ni Mratibu wa mradi SIDO Dodoma, amewafundisha wajasiriamali uhusiano wa Biashara na familia kwani mfanyabiashara asipokua makini na uhusiano huo anaweza kuua biashara wakati lengo lake ni kukuza mtaji kila wakati.
"Kuna tofauti kati ya mmiliki wa Biashara na Biashara yenyewe, hizi ni nafsi mbili tofauti zinazotakiwa kuheshimiana kwani unapokua na Biashara maana yake umejiari hivyo unapaswa kujilipa mshahara"
Naye Msimamizi wa Fedha kutoka SIDO Dodoma Bw. Justine Kahemela alipata nafasi ya kuwafundisha wajasiriamali hao namna ya kutunza fedha zinazotokana na Biashara kwa kununua bidhaa kwa bei za jumla na kujizuia kununua vitu vingi visivyokua na matumizi. "Unaweza ukanunua vitu vingi lakini hauvitumii na hii itapelekea kuyumbisha mtaji na hatimaye kuua biashara, jaribuni kununua vitu ambavyo vina matumizi ili kufanya mzunguko mzuri wa biashara ". Amesisitiza Bw. Kahemela.
Akifunga Mafunzo hayo ya siku moja, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Anthony Mtaka, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na uzalishaji Bi. Aziza Mumba, ameshukuru SIDO kwa kuwezesha Mafunzo hayo na amewakumbusha wajasiriamali hao kuwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Mtaka ameguswa na mahitaji yao na amependa kuwasaidia hivyo wasimuangushe katika kutimiza kiu yake ya kuwainua kiuchumi. Pia amewataka kuwa na dhamira ya kuwa na biashara kubwa zaidi, wasibaki hapo hapo wanapoanzia. MWISHO.
Comments
Post a Comment