"Sanaa na Utamaduni ni Ajira"- RC MTAKA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka ameeleza kuwa Sanaa, Utamaduni na michezo ni fani zinazotoa ajira kwa vijana na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi.
Mhe. Mtaka amesema hayo Julai 23, 2022 Chamwino Dodoma wakati
akifungua Tamasha la 13 la Muziki wa Cigogo linaloazimishwa kila mwaka.
"Nawaomba wazazi na walezi kuwaruhusu vijana wenu
kushiriki shughuli za Sanaa ,
utamaduni na michezo ni mojawapo ya ajira ambazo zinachangia
katika pato la taifa"amesema Mhe. Mtaka
Aidha Mhe. Mtaka ametoa wito
kwa waandaaji wa tamasha la
Cigogo kuliongezea thamani tamasha hilo ili lifikie kiwango cha kitaifa na
kimataifa kama lilivyo tamasha la Sauti
za Busara la Zanzibar.
Vilevile Mhe. Mtaka ametumia nafasi hiyo,kumpongeza
Mwanzilishi wa Tamasha hilo Dkt. Kedmon Mapana kwa kuaminiwa na Mhe. Samia
Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) ambapo amemsihi kuendelea kukuza sanaa kwakua ni kazi ambayo anaijua
vyema.
Pia Mhe. Mtaka amewataka wananchi kujitokeza kushiriki zoezi
la Sensa Agosti 23,2022 ili kupata takwimu sahihi kwa maendeleo ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa Dkt. Emmanuel Ishengoma
ameeleza kuwa dhamira ya wizara hiyo ni
kuhakikisha inafanya mageuzi ya Sanaa na Utamaduni kwa kuwa ni Sekta
muhimu zinazotoa ajira kwa vijana na kuchangia
katika uchumi wa nchi.
Tamasha la Cigogo linafanyika kwa siku tatu Julai 22 hadi 24,2022 likiongozwa na Kauli Mbiu "Elimu ya Sanaa ni Muhimu kwa Maendeleo Endelevu " linapambwa na ngoma mbalimbali za kitamaduni kutoka kabila la Wagogo Dodoma.
Mwisho
Comments
Post a Comment