"WIZARA TAFUTENI SULUHU YA MBWA WOTE WANAOZURULA MITAANI "-MHE.SENYAMULE



















Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipokuwa akizindua maadhimisho ya utoaji chanjo kwa mbwa na ili  kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa yaliyofanyika katika viwanja vya Mpunguzi Jijini Dodoma.

“Kila mtu ambaye anafuga mbwa lazima afuate sheria na taratibu zake, naagiza wataalamu wa mifugo wa Wizara na Sekretarieti kutafuta suluhu ya mbwa wote wanaozurura mitaani. Mtu kama hawezi kufuata sheria, aache kufuga wanyama hao”  Amesema Mhe. Senyamule

Mkuu wa Mkoa ameeleza, ugonjwa wa kichaa cha mbwa husababisha vifo 1500 kila mwaka nchini na Watoto chini ya miaka mitano ndio wamekuwa wahanga wakubwa zaidi. Hivyo, Serikali inatekeleza mpango mkakati wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kutoa chanjo hii kila mwaka ambapo mpaka sasa takribani mbwa 338,000 wameshachanjwa.

Mhe. Senyamule ametaja  lengo la Dunia ni kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030 kwa kuhakikisha kuwa kila mbwa anapatiwa chanjo kila mwaka. “Naomba utaratibu huu uwe endelevu mpaka ugonjwa huu uwe historia kwani Tanzania bila kichaa cha mbwa, inawezekana. Tunatakiwa kuzingatia chanjo pamoja na kupunguza idadi ya mbwa tunaofuga” Amesisitiza Mhe. Senyamule

Naye Mkurugenzi wa huduma za mifugo Profesa Hezron Nonga, amesema nchini Tanzania tuna mbwa takribani milioni 4.5 na paka milioni 2 wanaofugwa kwa malengo mbalimbali na kwa mwaka kuna wastani wa matukio 2,030 ya mbwa wanaodhaniwa kuwa na kichaa. Hivyo Shirika la Afya Dunia (WHO), Shirika la Afya za Wanyama duniani (WOAH) na Shirika la chakula na kilimo (FAO) kwa pamoja wamekubaliana kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030.

“Takwimu zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 60,000 hupoteza Maisha kwa kichaa cha mbwa duniani kila mwaka. Kwa Tanzania, kila mwaka wastani wa matukio ya majeraha kwa binadamu yanayotokana na kuumwa na mbwa ni 3,387 na hiin ni kwa mujibu wa ripoti ya WHO ya mwaka 2017.  Ugonjwa huu husababisha wastani wa vifo vya binadamu 1500 kila mwaka” Prof. Nonga

Maadhimisho ya utoaji chanjo kwa mbwa na paka hufanyika kila mwaka Duniani ikiwa ni kumuenzi muasisi wake Dr. Luis Paster ambaye ndiye aligundua chanjo hii kwa wanadamu na mbwa kwa mara ya kwanza mwaka 1885. Maadhimisho haya yanakwenda sambamba na utoaji wa chanjo ambapo kwa mwaka huu chanjo zaidi  ya 60,000 zenye thamani ya shilingi Milioni 180 zimetolewa, lengo ni kuchanja mbwa kwa zaidi ya asilimia 70.

Aidha, maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu inayosema, “Kichaa cha mbwa, afya moja, vifo sifuri” ikiwa na lengo la kutokomeza kabisa vifo vya binadamu vinavyotokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WA HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA WATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

‘WANAWAKE NA SAMIA’ 3000 MKOA WA DODOMA KUPATA MAFUNZO VETA