"Hela za Lishe zifanye Shughuli za Lishe "Dkt. Fatuma Mganga
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatuma Mganga ameyasema hayo wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa Viashiria vya Mkataba wa Lishe robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023, taarifa ambayo hutolewa kila baada ya miezi mitatu. Taarifa hii ni ya kipindi cha Julai hadi Oktoba 2022.
Dkt. Mganga amesisitiza kuwa vikao vya lishe viwe vikao
vinavyoleta tija, kwani suala la lishe ni suala mtambuka.Tunapaswa kutoa
taarifa sahihi ambazo zinaonyesha uhalisia.
Akitoa taarifa ya robo mwaka Bi. Adela Mlingi ameeleza kuwa
Mkoa wa Dodoma una jumla ya shule 947 (shule za msingi na sekondari ), kati ya
shule hizo 947, shule 830 ndizo
zinazotoa chakula shuleni hii ikiwa sawa na 87.6%.
Akikazia umuhimu wa Watoto/wanafunzi wote kupata uji au
chakula wakiwa shuleni, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma amewaelekeza wakurugenzi
wa halmashauri zote saba za mkoa kuongea na wazazi wa wanafunzi kwenye
Halmashauri zao ili kuja na utaratibu wa kuhakikisha angalau wanafunzi hao wanapata
uji wa saa 4.00 asubuhi.
Aidha Dkt. Mganga amewakumbusha wakurugenzi na wadau wa Lishe
kuwa tunaelekea msimu wa kilimo hivyo ni vyema shule zote za msingi na
sekondari zikaandaa maeneo ya kulima, kuaanda mbegu za mtama mweupe, kunde,
maharage na mahindi na kisha wanafunzi wapewe maeneo ya kulima ambapo chakula
kitakachopatikana kitakuwa kwa matumizi ya shule. Pia Katibu Tawala Mkoa
amewataka wakurugenzi kuwahusisha wadau kama WFP ambao wanaweza kuwapatia mbegu bora.
“Kila Mkurugenzi aje na mkakati wa jinsi watoto wanavyoweza
kula shuleni, Msimu huu wa kilimo shule zetu zote tulime, na tutafanya ukaguzi
kwa kila halmashauri ”.Ameagiza Dkt.Mganga.
Hali kadhalika wadau walipata fursa ya kuwasilisha taarifa za
Taasisi zao za robo mwaka ambapo Bi. Edina Paul amewasilisha taarifa ya
COUNSENUTH, kwa kueleza kuwa taasisi ya Counsenuth ilianza kazi 2018 na
inafanya kazi katika vijiji 114 na kata 26 za Wilaya ya Chemba, ambapo shughuli
zao kubwa ni kupambana na udumavu kwa vitendo. Taasisi hiyo imekuwa ikiendesha
semima na warsha lakini pia wamekuwa wakiendesha elimu ya lishe kwa vitendo kwa
kusisitiza wanafunzi walime mboga mboga mashuleni, kuhamasisha elimu ya afya kwa
mama na mtoto.
Mdau, Doctors with Africa- Cuamm, taasisi inayojishunghulisha
na lishe Wilaya ya Kongwa na Chamwino. Bi Flora Manyanda, ameeleza kuwa zaidi
ya robo tatu ya gharama zao hutumika kwa ajili ya gharama za chakula na Dawa.
Baada ya uwasilishaji wa mada hizo mbili, mwenyekiti wa kikao
hicho Katibu Tawala Mkoa amewataka wadau kuelekeza fedha zao kwenye jambo /suala la lishe badala ya kutumia kiasi
kikubwa cha fedha kwenye masuala ya posho.
“Tupunguze posho,na msisitizo uwe katika kutatua changamoto za
lishe, watoto wanywe maziwa pia tuwe na mikakati ya kuhakikisha watoto wanakula
shuleni, tuandae mbegu za kutosha za Mtama, Kunde, maharage, tukivuna tukaushe
kwa matumizi ya baadae. Watoto wakipata uji au chakula shuleni itasaidia
kupunguza utoro wa wanafunzi na kuongeza taaluma”. Amesisitiza Dkt. Mganga .
Aidha Dkt. Mganga amewataka wakurugenzi kuwakumbusha waalimu mashuleni
uwepo wa ratiba ya vipindi vya dini.
“Walimu wanatakiwa kuhakikisha vipindi vya dini vinakuwepo kwenye ratiba na vinafundishwa kama vipindi vingine vya hesabu au Jiografia. Viongozi wa Dini Msisitie kuendelea kuwafundisha watoto wetu maadili ya mwenyezi Mungu. Kwa kufanya,hivyo mtakuwa mkitengeneza jamii bora ya kesho.”
MWISHO.
Comments
Post a Comment