SOKO LA MACHINGA KUANZA RASMI OKTOBA 30





















Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amefanya kikao na machinga wanaotarajiwa kufanya biashara katika soko la machinga lililopo barabara ya Bahi, lengo kuu likiwa kusikiliza na kutatua  kero zao.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa ameongozana na Katibu Tawala Mkoa Dkt. Fatuma Mganga, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Mhe. Jabir Shekimweri, Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya pamoja na viongozi wanaosimamia soko hilo kutoka katika Halmashauri ya Dodoma Jiji.

Mkuu wa Mkoa, ameanza kikao kwa kusikiliza kero kadhaa zinazowakabili machinga hao wakati wakisubiri kuhamia katika soko hilo. Miongoni mwa kero hizo ni pamoja na baadhi ya wafanya biashara kupangiwa vizimba ambavyo haviendani na biashara zao, baadhi ya machinga kukosa mikopo, machinga wa vitabu na magazeti kukosa vizimba, baba na mama lishe kukosa vizimba, daladala kushusa abiria eneo hilo, n.k

Kero hizo zimepata majawabu kutoka kwa kaimu Mkurugenzi wa Jiji Bw. Msangi pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu uhakiki wa Machinga Bw.Joseph Bulali, ambaye alijibu hoja zilizojikita kwenye changamoto ya mama na baba lishe, vitambulisho vya machinga, maeneo ya wazi baada ya soko kufungwa, pamoja na ushuru.

Akijibu changamoto ya baadhi ya machinga kukosa mikopo, katibu wa Soko la Machinga Bi. Sigirinda Mtemu, amesema kuwa, halmashauri zote zimekuwa zikitoa mikopo ya 10% kutokana na mapato ya ndani, mikopo ambayo mgawanyo wake ni 4% vijana, 4% wanawake na 2% watu wenye ulemavu. Sifa/kigezo cha kuwawezesha vijana  kupata mkopo ni pamoja na umri ambao ni miaka 18-35, vijana hao wanatakiwa wawe kwenye vikundi vya watu watano watano.Mpaka sasa tumevitambua vikundi 103 kila kikundi kikiwa na watu watano watano pamoja na watu wenye ulemavu 7.

Changamoto ambazo tunakutana nazo katika utoaji wa mikopo  hiyo ni kuwa baadhi ya watu wameunda vikundi vya watu 5 ambapo ndani ya kundi hilo hakuna machinga hivyo kuwia vigumu kuwapatia mikopo hiyo.

Moja ya changamoto ambayo imeelezwa na machinga hao ni kuhusu wateja wao ambao wengi wanatoka vyuo vya UDOM, MIPANGO, ST. JOHN, na eneo la Nzuguni na hivyo kumuomba mkuu wa mkoa kuwa mabasi ya kutoka maeneo hayo yawe yanafika kwenye kituo hicho kipya kitakachokuwa eneo la Machinga Complex.

 Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Mkoa amewataka LATRA kuhakikisha kuwa  kufikia tarehe Mosi Novemba, daladala zinapita njia ya  soko hilo na kunakua na kituo cha kupakia na kushusha abiria.

Mbali na majawabu ya kero, Mhe. Senyamule ametoa maagizo ya Serikali kwa kuwataka machinga hao kuwa tayari kuhamia kwenye soko hilo.



“Machinga tuwe tayari kuhamia hapa, tunakwenda kufanya biashara. Natoa wito kwenu tulitunze jengo hili kwani limegharimu fedha nyingi. Tufanye biashara kwa uaminifu na uadilifu, pasiwepo kuibiana na tutunze usafi wa mazingira” Amesisitiza  Mhe.Senyamule.

Aidha, amewataka Halmashauri ya Jiji kutatua kero zote zilizojitokeza na ambazo zitajitokeza hapo baadae “Jiji endeleeni kutatua kero hizi na zitakazojitokeza kwani maeneo bado yapo mengi endapo kama kutajitokeza upungufu wa vizimba watapangiwa maeneo mengine. Tunatamani kuiona Dodoma ambayo ni Fahari ya Watanzania  na soko hili tayari ni Fahari”

Vilevile, Mkuu wa Mkoa ametangaza rasmi tarehe ya machinga kuanza kuhamia kwenye soko hilo, ambayo ni kuanzia tarehe 28, 29 na 30 Oktoba, 2022 huku akiwataka viongozi wa Halmashauri ya Jiji kukaa eneo hilo siku zote hizo kwa ajili ya usimamizi wa zoezi hilo.

Naye Katibu Tawala Mkoa Dkt. Fatuma Mganga, amesema kuwa Dodoma tumebahatika kupata soko zuri na kuwataka machinga wasisite kuhamia sokoni hapo kwani milango ya kutatua changamoto haijafungwa. Pia amezungumzia suala la mikopo kwa wafanya biashara wadogo wadogo.

“Kuna mifuko zaidi ya 69 inayotoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, pia kuna mabenki. Mutakapohamia hapa na kufahamika kwamba mnapatikana hapa kwa pamoja, mifuko hii pamoja na benki hizi zitawafuata hapa kuwahudumia. Naamini tunakwenda kuhamia kwa utulivu na Jiji letu linakwenda kuwa safi” Dkt. Mganga

 

MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA