''CHUO CHA UFUNDI DONBOSCO, MFANO WA KUIGWA"RC SENYAMULE
Chuo cha Ufundi Don Bosco Mkoani Dodoma ni Chuo cha Ufundi Stadi,ambacho kipo chini ya Kanisa Katoliki. Hivi karibuni Chuo hicho kimefanya mahafali yake ya 36 ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Mahafali hayo yamejumuisha
wahitimu 213 ambapo ni mchanganyiko wa wale waliokua wakisoma kozi ndefu na
wengine kozi fupi katika fani ya umeme, kilimo, ufundi bomba, ufundi magari, uchomeleaji,
mapishi, seremala, ushonaji n.k
Mhe. Senyamule amekipongeza chuo
hicho kwa kuwa mfano wa kuigwa. “Don Bosco mmekua mfano kwa kushiriki katika
michezo, uwezeshaji wa vifaa vya kufanyia kazi kwa wanafunzi wanaohitimu pamoja
na kushirikiana na Serikali hususani Ofisi ya Waziri Mkuu Watu wenye ulemavu. Hongereni
sana. Watu wenye ujuzi ndio wenye uwezo wa kufanya mabadiliko katika jamii.
Serikali ina uelekeo wa kuwa na viwanda vingi ambayo vinahitaji wataalamu wenye
ujuzi hivyo hata Halmashauri zetu zimeelekezwa kuwawezesha wanafunzi
wanaomaliza vyuo vya ufundi” RC Senyamule
Pia ameongeza kuwa Serikali
imeendelea kutengeneza fursa mbalimbali kwa vijana kama vile kuziamuru
halmashauri kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi yenye uhitaji kwenye jamii
wakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hivyo amewataka wahitimu hao
kujiunga kwenye vikundi ili nao waweze kuwa wanufaika wa mikopo hiyo
itakayowawezesha kujiajiri kwa ujuzi walioupata chuoni hapo.
Bi. Prisca Byala, Afisa Elimu
Msingi ambaye amemuwakilisha Afisa Elimu Mkoa katika Mahafali hayo, amesema
mafunzo haya ni hazina kwa vijana na Taifa kwa ujumla na anaamini kuwa
yatawanufaisha huko wanapokwenda hivyo hakusita kuishukuru Serikali kwa kuyapa
kipaumbele mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana.
Kadhalika akiongea kwa niaba ya
uongozi wa Chuo, Mkuu wa chuo hicho Mkoa wa Dodoma Father Boniface Mchami,
amesema “Chuo kinawalea vijana katika maadili mema na ucha Mungu, chuo kina
ushirikiano na vyuo vingine kupitia michezo, semina na shughuli mbalimbali.
Tumefadhili vijana 67 wanaosoma hapa ambao hawana uwezo wa kulipa ada pia Chuo
kimepata nafasi ya kushirikiana na kampuni 5 kutoka nchini Marekani
zinazojishughulisha na uchimbaji wa mafuta na wametoa scholarship kwa wanafunzi
wetu 10 pamoja na walimu wanne kwenda kwenye mafunzo ya mwaka mmoja nchini
Marekani”. Amesema Father Mchami
MWISHO
Comments
Post a Comment