WATOTO 695,508 KUPATA CHANJO YA POLIO MKOANI DODOMA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
chini ya Idara ya Afya, imefanya kikao cha kamati ya afya msingi ikiwa ni
katika kuhamasisha awamu ya nne ya utoaji wa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Polio
kwa Watoto wenye umri kuanzia miaka 0 hadi miaka 5. Chanjo hiyo itaanza kutolewa tarehe 1 Desemba mpaka 4, 2022.
Chanjo hii kama ilivyokua
ikitolewa kwenye awamu zilizopita, inatarajiwa kutolewa nyumba kwa nyumba ili
kuweza kufikia idadi kubwa ya Watoto wenye uhitaji wa huduma hiyo ambapo
matarajio ni kuchanja Watoto 695,508.
Akihamasisha wazazi kushiriki kikamilifu kuwatoa Watoto wao wapate chanjo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema; “Dodoma tumefanya vizuri katika awamu zilizopita na leo tunajadili namna nzuri ya kwenda kutekeleza awamu hii ya nne. Mhe.Rais ametimiza wajibu wake kwa kutoa fedha na sisi tutekeleze jukumu hili. Nasisitiza chanjo ni salama, wazazi andaeni Watoto wote. Ni imani yangu tutakwenda kutoa elimu tutakayoipata hapa kwa wazazi wenye Watoto wenye umri kuanzia miaka 0 hadi miaka 5. Wazazi mtafuatwa nyumba kwa nyumba Watoto wachanjwe, kwani Dodoma bila Polio inawezekana” RC Senyamule.
Kadhalika Katibu Tawala Mkoa wa
Dodoma Dkt Fatma Mganga, amewaomba viongozi wa dini kuwatangazia waumini wote
kuhakikisha Watoto wenye umri wa miaka 0-5 wanapata chanjo.Na kuwataka Wachanjani kufika maeneo ya
ibada ambayo wazazi watakuwa pamoja na Watoto wao kwani tarehe 02/12 ni ijumaa
na tarehe 04/12/2022 ni jumapili na wazazi wengi watakuwa maeneo ya ibada.
Aidha Dkt. Mganga ametoa shime
kwa wachanjaji kuangalia muda mujarabu ambao wanaweza kuwakuta wazazi pamoja na
watoto nyumbani kwani hivi karibu tunatarajia majira ya mvua na hivyo wazazi
wengi watakuwa mashambani na Watoto wao.Hivyo ni vyema kwenda muda wa jioni
ambapo watakuwa wametoka mashambani.“Tunatamani Watoto wetu wote wajitokeze ili
tutokomeze Polio mkoa wa Dodoma” Dkt. Mganga
Vilevile, Afisa Afya Mkoa wa
Dodoma anayesimamia zoezi hili Bw. Francis Bujiku, ametoa taarifa ya utoaji wa
chanjo hii ya awamu ya nne.
“Awamu ya nne itafanyika kwa siku
nne kuanzia Desemba 1 mpaka 4, 2022 ambapo zoezi hili litakwenda sambamba na
utoaji wa huduma zingine ikiwemo elimu ya chanjo. Walengwa wa kampeni ya sasa
ni Watoto 695,508. Kuna jumla ya chanjo 765, 059 zilizotolewa, huku bajeti ya
utoaji chanjo hii kwa ngazi ya Mkoa ikiwa ni kiasi cha shilingi 45,524,000.00”
Bw. Bujiku.
Ugonjwa wa Polio umekua tishio
kwa miaka mingi katika nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania. Mara ya mwisho
nchi yetu ilipata mgonjwa mwezi Julai mwaka 1996. Hivi karibuni nchi ya Malawi
ilitoa taarifa ya mgonjwa wa Polio mnamo tarehe 17 Februari, 2022 katika mji wa
Lilongwe hivyo Tanzania ilionekana ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari
kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu na ndio sababu Serikali kupitia
Wizara ya Afya imefikia uamuzi wa kutoa chanjo hii kwa Watoto wote wenye umri
wa miaka 0-5 nchini.
MWISHO
Comments
Post a Comment