DODOMA YAJIPANGA KUKABILIANA NA
UTORO SHULENI 2023
Mkoa wa Dodoma umejidhatiti
kukabiliana na utoro wa wanafunzi shuleni kupitia maazimio yaliyowekwa kwa
mwaka 2023 kupitia kikao cha pili cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa kilichofanyika
katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jengo la Mkapa chini ya Mwenyekiti wake
Mhe. Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Katika kikao hicho, agenda ya
elimu imejadiliwa kwa kina na kupewa msukumo madhubuti ikiwa ni miongoni mwa
ajenda nane za kikao hicho kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo
ikiwemo bajeti ya Mkoa, Elimu, Afya, Kilimo, Maji na Mazingira.
Mkoa wa Dodoma unakabiliwa na
changamoto kubwa ya utoro kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari huku
sababu kubwa zikitajwa kuwa ni ukosefu wa chakula shuleni, Wazazi/Walezi
kutoipa thamani stahiki elimu hivyo kutowajibika kwa malezi ya watoto wao, Viongozi
wa Vijiji kushindwa kutimiza wajibu wao wa kudhibiti utoro shuleni na umbali
mrefu wa kwenda na kurudi.
Akizungumza katika kikao hicho,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema licha ya changamoto hizo
katika sekta ya elimu, Wilaya ya Bahi imefanikiwa kushika nafasi ya kumi
kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2022.
“Naipongeza sana Halmashauri ya
Bahi kwa kushika nafasi ya kumi kwa mpangilio wa ufaulu wa Halmashauri kitaifa
kwani wameifaharisha Mkoa mzima wa Dodoma. Natoa shime kwa Halmashauri nyingine
kwenda kujifunza Bahi namna walivyofanya na kufanikiwa kuingia kwenye kumi bora
za kitaifa. Pia tukafanye kazi kubwa kuhakikisha watoro wanarudi shuleni mwaka
2023” Amesema Mheshimiwa Senyamule.
Kwa upande wake, Katibu Tawala
Mkoa Dkt. Fatuma Mganga naye ametoa rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa
wa Dodoma kutoa msukumo kwa walimu kufundisha kwa bidii kwa lengo la kuongeza
kiwango cha ufaulu.
Akitoa maoni yake juu ya maazimio
ya mwaka 2023, Afisa Elimu Mkoa Bw. Gift Kyando amesema “Mwaka ujao tunaazimia
wanafunzi wote watakaomaliza elimu ya msingi kurudi mapema shuleni kwa ajili ya
kujiandaa na masomo ya kidato cha kwanza tofauti na ilivyokua mwaka huu kwani
mitihani ilichelewa badala ya kufanyika mwezi Septemba imefanyika mwezi Oktoba
ila mwakani itafanyika kama kawaida mwezi Septemba”
Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameziagiza Halmashauri kuongeze kasi ya
kukusanya mapato na kutoa asilimia kumi. “Naziagiza Halmashauri zote kwa
kushirikiana na wadau kuendelee kutengeneza madawati ili kupunguza upungufu
uliopo, Halmashauri zikamilishe usimamizi wa sheria ndogondogo za upatikanaji
wa chakula shuleni pamoja na kudhibiti utoro, kila shule itenge eneo la
kuzalishia chakula kwa wanafunzi, vyuo vya ufundi viimarishwe” Alisisitiza Mhe.
Senyamule.
MWISHO
Comments
Post a Comment