WASIOPANDA MITI KWENYE MAENEO YAO KUCHUKULIWA HATUA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na wadau wa
mazingira, leo tarehe 30 Desemba 2022, imetangaza kampeni maalumu ya upandaji
miti katika Mkoa wa Dodoma lengo hasa likiwa ni kutimiza lengo la kampeni ya
kuikijani Dodoma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary
Senyamule alipokua akizungumza na waandishi wa Habari kwenye ukumbi uliopo
kwenye jengo la Mkapa, ofisini kwake.
“Sote tunafahamu kuwa msimu wa mvua umeanza hivyo, ni wakati
sahihi kwa wananchi na wakazi wote wa Dodoma kutekeleza kwa vitendo Kampeni ya
upandaji miti kuanzia ngazi ya Kaya, Kata, Vijiji, Vitongoji hadi ngazi ya Taasisi na msisitizo wa mwaka
huu ni kwamba miti yote itakayopandwa hakikisheni inakua na kustawi vizuri”
Amesisitiza Mhe. Senyamule
Kadhalika, Mkuu wa Mkoa amezitaja baadhi ya faida za uwepo wa
miti ya kutosha katika mazingira yetu na Mkoa kwa ujumla kuwa ina mchango
mkubwa katika maendeleo ya uchumi na jamii kwa ujumla kwani misitu inatoa
asilimia 45 ya malighafi za ujenzi, hunyonya hewa ukaa, hutupatia hewa safi,
kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji na pia huchangia ongezeko la pato la
Taifa.
“Ninafahamu wenzetu wakala wa misitu TFS wamezalisha miche ya
miti ya kutosha pale katika kitalu cha miti eneo la Mailimbili na miche
hiiinagawiwa bure, hivyo natoa rai kwa wanadodoma kufika pale kuchukua miche ya
miti na kupanda katika maeneo yenu. Tutapita kukagua kila nyumba na kuona miti
mitano iliyopandwa na wale wasiopanda watachukuliwa hatua kwa kuwa hii ni
sehemu yasheria ndogo tulizonazo kwenye Halmashauri” Ameongeza Mh. Senyamule
Kampeni ya upandaji miti Mkoa wa Dodoma inayotarajiwa kuanza
Desema 31hadi msimu wa mvua utakapokwisha, imelenga Halmashauri zote nane za
Mkoa kwani lengo kuu la Mkoa ni kila Halmashauri kupanda miti 1,500,000 kwa
mwaka licha ya baadhi ya maeneo kupewa kipaombele kama eneo la Ihumwa kwenye
chanzo cha maji cha DUWASA na katika bonde la Mzakwe.
Comments
Post a Comment