KATIBU TAWALA MKOA WA DODOMA DKT. FATUMA MGANGA AFUNGUA MAFUNZO YA PROGRAM YA SHULE BORA KWA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA DODOMA
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dkt Fatuma Mganga ametoa rai kwa waandishi wa habari wanaofanya kazi ndani ya Mkoa huo kutangaza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu pamoja na kuyatangaza kwa jamii.
Rai hiyo ameitoa Januari 27, 2023 Wilayani Kondoa wakati akifungua mafunzo ya Siku Moja kwa maafisa habari na waandishi wa habari, yenye lengo la kuwajengea uwezo kufahamu Mradi wa Shule Bora na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu Katika masuala ya elimu.
Akizungumzia suala la maendeleo ya Elimu Katika Mkoa amesema suala la Elimu katika Mkoa wa Dodoma bado halijatangazwa vizuri na kuwataka waandishi wa habari wakawe chachu cha kuielimisha jamii.
Pia amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati za kuongeza pesa za maendeleo katika mkoa wa Dodoma ambapo shilingi bilioni 7.8 zimetolewa na kuwezesha kujenga vyumba vya madarasa 393 kwa Shule za Msingi na madarasa 130 yamejengwa kwa Shule za Sekondari yamejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 20
Aidha amewaeleza waandishi wa habari kuwa Rais Samia ameongeza bajeti ya Elimu bila malipo kwa Shule za Misingi na Sekondari.
Pamoja na jitihada hizo za serikali amewataka wazazi kushirikiana na serikali katika ujenzi na uhifadhi wa Miundombinu ya elimu ikiwemo ya madarasa ambapo ameeleza Mkoa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 7000, ambapo mwaka huu peke yake wanatarajia zaidi ya wanafunzi elfu 90 kuanza masomo.
Aidha amewaomba wazazi wawapeleke watoto shule, wasiwafiche na kuwatumikisha Shughuli za kilimo na kazi za ndani.
Mbali na hilo amekemea dhana iliyozoeleka kwamba Mkoa wa Dodoma ni wa kutoa Wasaidizi wa Shughuli za ndani.
Mpaka kufikia Januari 26 , 2023 ni asilimia 89.7 ya wanafunzi wa madarasa ya awali wameripoti shule, asilimia 94.2 Kwa darasa la kwanza na asilimia 66.95 kidato Cha kwanza.
“Mwisho nawaomba waandishi wa habari
mkasaidie kutangaza mafanikio ya Mkoa yaliyopatikana katika sekta ya elimu, ili
jamii iweze kuyafahamu pia kurahisisha serikali kuendelea kutuunga Mkono katika
jitihada zetu hizi”. Alisema Dkt. Mganga
Comments
Post a Comment