MKOA WA DODOMA WAAINISHA MAKUBWA YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA, YATANGAZA MAFANIKIO YAKE










Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango amehimiza wananchi wa Dodoma kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa Mkoa na nchi nzima kwa ujumla.

Dkt. Mpango ameyasema hayo leo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angela Kairuki katika ukumbi wa Kanisa la TAG - Mipango katika Mkutano wa kutangaza Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Serikali kwa kipindi cha Miaka Miwili (2021/2022- 2022/2023) 

"Licha ya anguko la kiuchumi Duniani kufuatia ugonjwa wa UVIKO - 19 pamoja na vita inavyoendelea huko Ukraine, bado uchumi wetu umeendelea kukua na tunatarajia kufikia hadi 5.0% na Dodoma inakua na kuchangia 3.1%ya pato la Taifa. Nawahimiza wananchi wa Dodoma kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha mchango wao katika pato la Taifa unaendelea kukua" Amesisitiza Mhe. Mpango.

Kadhalika, ameongelea pia suala la elimu kwa kusisitiza wazazi na walezi kupeleka watoto shule. " Tuhamasishe upatikanaji wa chakula mashuleni ili wanafunzi wetu watulie na kusoma vizuri. Tuwape ushirikiano walimu wanafanya kazi kubwa ya kuliandaa taifa la kesho na kuwapa motisha kila wanapofanya vizuri. Tutaendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu. Tuhimize wazazi wapeleke watoto shule na kila Kiongozi kwa nafasi yake awajibike kuhakikisha kila mtoto anakwenda shule" Alisisitiza Mhe. Makamu wa Rais.

Akiwasilisha mafanikio ya Mkoa wa Dodoma kupitia miradi kwenye sekta ya elimu, Mkuu wa Mkoa Mhe. Rosemary Senyamule amesema,"Kwa upande wa elimu, idadi ya vyumba vya madarasa kwa shule za msingi imeongezeka kutoka madarasa 5,812 yaliyokuwepo mwaka 2020/21 hadi kufikia madarasa 6,205 mwaka 2022/23. Ongezeko la madarasa 393 limewezesha wanafunzi kusomea madarasani na kwa nafasi. Vyumba vya madarasa kwa sekondari pia vimeongezeka kutoka 2,226 hadi kufikia 3,256 ambapo ni ongezeko la madarasa 1,030. 

Pia uwekezaji Mkubwa wa Serikali katika chuo kikuu cha Dodoma, usajili wa wanafunzi umeendelea kukua kutoka wanafunzi 1,200 mwaka 2007 hadi kufikia 30,891 katika mwaka wa masomo 2021/22 wakiwemo wanafunzi kutoka nje ya nchi" 

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga amesema Mkoa wa Dodoma umebarikiwa ardhi ya kutosha kwa ajili ya shughuli za kilimo na amewahimiza wananchi kuwekeza kwenye sekta ya kilimo kwani asilimia kubwa ya wananchi wa Dodoma wanategemea kilimo kuendesha maisha yao. 

"Mkoa wetu umebarikiwa ardhi ya kutosha kwa ajili ya kilimo kwani tuna ardhi yenye ukubwa wa Hekta Milioni 4.1 ambapo eneo la Hekta Milioni 2 linafaa kwa kilimo ingawa ni eneo la Hekta Milioni 1.2 tu ambalo ni sawa na 62% ndilo linatumika kwa kilimo kwa Sasa. Vilevile kwa upande wa mifugo, Mkoa wetu ni miongoni mwa mikoa mitatu inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mifungo kwani tuna mifungo inayofikia Milioni 2.7 Niwahimize wananchi wa Dodoma kuwa maendeleo yanahitaji watu, hatuna sababu ya kulalamika kwani tumeshabarikiwa vitu vyote na viongozi tunapaswa kujitafakari kwa hili" Dkt. Mganga. 

Kufuatia juhudi kubwa za viongozi kuleta wawekezaji kwenye Mkoa wa Dodoma, tunatarajia kuiona Dodoma kama Mkoa wenye mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza Dodoma kuanzia wa ndani hadi wa nje ili kuongeza kasi ya uwekezaji kwa Mkoa, Wilaya na Vijiji pia kujenga imani kwa wawekezaji na kuweka vivutio kwa wawekezaji wa kimkakati.

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA