MRADI WA REST WAZINDULIWA DODOMA
Mkoa wa Dodoma umezindua rasmi
mradi unaoshughulikia masuala ya afya ya uzazi kwa vijana, wanawake na watoto
unaojulikana kama Reproductive Equity Strategic (REST) unaoendeshwa na shirika
lisilo la Kiserikali la Deutsche Shiftung Weltbevolkerung (DSW) - Tanzania
ambao utafanya kazi kwenye Wilaya tatu za Mkoa ikiwa ni pamoja na Dodoma mjini,
Bahi na Mpwapwa. Mradi huo umezinduliwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Rosemary Senyamule
kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa jengo la Mkapa.
Akizindua mradi huo Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetoa
kipaumbele katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu yake
ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora ya afya.
“Matokeo ya sensa ya mwaka
2022 yanaonyesha kuwa Tanzania ina jumla ya hospitali 676, vituo vya afya 1,466
na zahanati 7, 965. Tanzania Bara pekee ina hospitali 662, vituo vya afya 1,430
na zahanati 7,680 na mkoa wetu wa Dodoma una vituo vya afya 69 na zahanati 402.
Hivyo ni muhimu sana kuendelea kuhamasisha wananchi hususan wakina mama
wajawazito kutumia vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma, mpango wa
Serikali ni kutokomeza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ifikapo
mwaka 2025” Amesema Mhe. Senyamule
Mheshimiwa Senyamule ametoa
rai kwa waratibu na watekelezaji wa mradi huu kuweka malengo ya kufika kata
nyingi zaidi za Mkoa wa Dodoma kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi.
“Mradi huu unafanya kazi
kwenye Kata 17 tu za Halmashauri hizi tatu, wakati Dodoma ina kata nyingi
zaidi, tupange mkakati wa kuzifikia kata nyingi zaidi za mkoa ili muwe mfano wa
kuigwa na kuvutia wengi zaidi kuwekeza Dodoma. Nitoe rai, mkafanye kazi kwa
ufanisi mkubwa maana tunataka kila unachokifanya Dodoma, kifanyike kwa ufanisi kwani
tunakwenda kuifaharisha Dodoma kwa mradi huu” Ameongeza Mhe. Senyamule
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Shirika la DSW Bw. Peter Owaga, amesema “mradi huu unatekelezwa kwenye mikoa
minne ya Tanzania ambayo ni ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na
kwa mkoa wa Dodoma unatekelezwa katika Wilaya tatu ikiwemo Dodoma mjini, Bahi
na Mpwapwa chini ya mashirika ya DOYODO, WOWAP na FAEAF wakiongozwa na Shirika
la DSW Tanzania
Lengo la mradi huu ni
kuwajengea uwezo asasi zisizo za kiserikali na kusaidia wanawake na wasichana
wanapata na wanatumia huduma za afya ikiwemo afya ya uzazi ili kuleta ustawi
wao na kuweza kutimiza matarajio na malengo ya maisha yao. Mradi huu pia
utasaidia utekelezaji wa sera na miongozo mbalimbali ya afya ya uzazi ikiwemo
kupinga unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na
watoto.
MWISHO
Comments
Post a Comment