UKILETWA DODOMA UMELETWA KUJENGA MAKAO MAKUU YA NCHI
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary
Senyamule amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald R. Mongella pamoja
na kuwapokea Wakuu wa Wilaya wapya wawili waliohamishiwa Mkoa wa Dodoma kwenye
hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa jengo la Mkapa zilipo Ofisi za Mkuu wa
Mkoa.
Mhe. Senyamule amewaasa Wakuu
hao wa Wilaya kuheshimu nafasi waliyopewa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
kwani wameaminika kuitumikia nafasi hiyo. “Nafasi ya Ukuu wa Wilaya ina madaraka
na dhamana kubwa sana, ukiyatumia kwa tija yanaleta manufaa ila ukiyatumia
vibaya utakwenda kupata matokeo mabaya”
Aidha Mhe. Senyamule amesema
kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi na nafasi waliyopewa wakuu hao ni kuja kuijenga Makao Makuu.
“Kuja Dodoma ni bahati kwakuwa
mnakuwa sehemu ya kujenga Makao Makuu ya nchi. Yeyote aliyekuja hapa, ajue
amepata nafasi ya kujenga Makao Makuu kwani viongozi wetu wakuu wana matarajio
makubwa na sisi. Mkoa umejipanga kuifanya Makao Makuu kama yalivyo matarajio ya
viongozi wetu” Mhe. Senyamule
Vilevile Mhe. Senyamule
amegusia changamoto zinazoukabili Mkoa wa Dodoma kwenye sekta ya elimu ikiwemo
utoro, ufaulu hafifu, ukosefu wa chakula shuleni na upungufu wa miundombinu ya
elimu na kuwaagiza Wakuu hao wapya kwenda kusimamia kikamilifu utatuzi wa changamoto
hizo kwa kushirikiana na watendaji na wenyeviti wa Vijiji na Kata.
“Halmashauri zetu zina
changamoto kubwa kwa upande wa elimu ambazo tunajitahidi kukabiliana nazo kwa
mwaka huu. Kwenye upungufu wa miundombinu, nimetoa maagizo kwa wenyeviti wa
Kata na Vijiji kukaa vikao na kukubaliana kujenga maboma mawili kwa kila Kijiji
kwa mwaka, nendeni mkasimamie agizo hili” Amesisitiza Mhe. Senyamule
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa
Dodoma Dkt. Fatuma Mganga, amepata fursa ya kutoa neno kwa Wakuu hao wapya wa
Wilaya wakati wa hafla hiyo;
“Bahi imejipambanua vizuri kwa
elimu, miradi na mambo mengine mengi hivyo tunaamini Mkuu wa Wilaya Mpya
atakwenda kuendeleza hayo. Wilaya ya Mpwapwa bado ipo nyuma kwenye
uandikishwaji wa wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza mwaka huu hivyo
tunategemea utakwenda kuhimiza zaidi. Tunategemea Wilaya iwe na vitendo Zaidi
kuliko nadharia” Dkt. Mganga
Katika salamu zao za shukrani,
wakuu wa Wilaya ya Chemba na Mpwapwa wameahidi kufanya kazi kwa weledi na
uaminifu kama viapo walivyoapa vinavyowataka huku wakitekeleza ilani ya Chama
Tawala pia wamesema kuwa dhamana waliyopewa ni deni kwa Mhe. Rais aliyewaamini
kwa kuwapa na fasi hizo na wanapaswa kulilipa. Wameahidi kuviishi viapo vyao na
kwenda kutekeleza maagizo yote ya Mkuu wa Mkoa huku wakiwa tayari kutumika
wakati wowote.
Uapisho huo umekwenda sambamba
na kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Munkunda
aliyehamishiwa katika Wilaya ya Temeke
Mkoani Dar es Salaam. Wengine waliokaribishwa ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe.
Godwin Gondwe pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo.
MWISHO
Comments
Post a Comment