WANAWAKE SIMAMENI KWENYE NAFASI ZENU ZA MALEZI














Wito umetolewa kwa wanawake kusimama kwenye nafasi zao za malezi kwa watoto ili kutengeneza jamii yenye maadili. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule alipokuwa akitoa hotuba yake wakati wa Kongamano la wasichana wa Baraza la Kiislamu Tanzania BAKWATA lililofanyika kwenye eneo la Msikiti wa Gaddafi Jijini Dodoma.

Kongamano hilo lililoandaliwa na BAKWATA kwa wasichana, limelenga kujadili mambo mbalimbali yanayowakabili wasichana kwenye jamii hasa kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake katika jamii zetu.

"Wanawake tusimame kwenye nafasi zetu za malezi ya watoto kwani maadili yameharibika nyakati hizi ndio mana kuna wimbi kubwa la vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa watoto na wanawake. Tukishirikiana na kuamua kwa pamoja kutokomeza vitendo hivi, hakuna linaloshindikana" Amesema Mhe Senyamule

Aidha amefafanua suala la mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa kundi la wanawake na kuwaondolea hofu ya kwenda kukopa.

"Tutaandaa wadau watakaowapa darasa juu ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri. Ondoeni hofu ya kuchukua mikopo kwani kwenye manunuzi ya Serikali, Sheria imewekwa kwamba asilimia 10 ya manunuzi yafanyike kutoka kwenye vikundi vya wanawake wajasiriamali na Kwa Sasa Mkoa wetu una miradi mingi inayohitaji ununuzi wa vifaa, hivyo undeni vikundi, muende mukapate mikopo muanzishe biashara kwani wateja wapo ikiwemo Serikali" Mhe. Senyamule 

Vilevile, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma Bw. Mustapha Rajab Shaaban amezungumzia juu ya uhuru wa kuabudu kwa kusema;

"Serikali yetu haina dini na inatoa fursa kwa kila mtu kuabudu kwa imani yake ili mradi tu asivunje katiba. nitashangaa kuona watu wa dini tofauti wanagombana kisa utofauti wa Imani zao. Tuungane na Serikali kufanya ibada zetu huku tukidumisha Amani na utulivu" Sheikh Mustapha Shaaban.

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA