DUWASA YAJIPAMBANUA UHAKIKA WA MAJI DODOMA
Mamlaka ya maji safi na usafi
wa Mazingira Mkoa wa Dodoma (DUWASA) inaendelea kufanikisha lengo la
upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 kwa Mkoa wa Dodoma kufuatia juhudi za
Serikali ya awamu ya Sita. Hayo yamebainishwa wakati wa mfululizo wa vipindi
maalumu vya kutangaza mafanikio ya Serikali kwa Taasisi za Umma vilivyoandaliwa
na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambapo leo kimeangazia sekta ya maji.
Akiwasilisha
hotuba yake mbele ya wanahabari wakati wa utangulizi wa kipindi hicho, Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameelezea miradi mbalimbali ya maji
inayoendelea katika Mkoa na utekelezaji wake ndani ya kipindi hiki cha miaka
miwili ya Serikali ya awamu ya sita.
“Tunafahamu maji ni kila kitu katika maisha ya
mwanadamu, maji ni Uhai. Katika Mkoa wa Dodoma, kumekuwa na Uendelezaji wa vyanzo vya maji
(uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa) kwa kutumia vyanzo vikuu kama vile Uchimbaji
wa visima virefu 34, Ujenzi wa Mabwawa 2
ya maji, miradi 10 ya maji inayotumia mtandao wa bomba imekamilika, Uzalishaji wa Maji umeongezeka kutoka wastani wa lita
61.5 Milioni hadi lita 67.8 Milioni. Ongezeko hili la uzalishaji limetokana na
kukamilika kwa Miradi Mipya ya Maji yenye thamani ya Shilingi 9.14 Bilioni. Upatikanaji
wa huduma ya Maji vijijini kwa Mkoa wa Dodoma umefikia wakazi 1,393,167 sawa na
asilimia 65.1 na Lengo la Serikali ni kuhakikisha tunamtua Mama Ndoo
kichwani miradi ya maji inaendelea kila Wilaya ili kufikia 85% ya upatikanaji
wa maji vijijini ifikapo 2025” Amesema
Mhe. Senyamule
Akifafanua
mipango ya muda mrefu na wa kati ya Serikali kwa Mamlaka hiyo juu ya
kuhakikisha upatikanaji wa maji unakua wa uhakika kwa Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi. Aron Joseph amesema;
“Serikali
ina mipango ya kati ya kuhakikisha inamaliza tatizo la upatikanaji wa maji
ikiwemo mradi wa Bwawa la Farkwa katika Halmashauri ya Chemba unaogharimu kiasi
cha Dola za Kimarekani Milioni 793.5, mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria
ambapo upo katika hatua ya usanifu. Pia kuna mpango wa dharura wa kuchukua maji
kutoka Bwawa la Mtera lita Milioni 130 kwa siku sawa na asilimia moja ya maji
yanayozalisha umeme ambayo yatasambazwa Dodoma nzima na mradi huu utagharimu
kiasi cha Shilingi Bilioni 326” Amesema Mhandisi. Aron
Vilevile
Mkurugenzi huyo ameainisha baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo katika
utendaji wao wa kazi ikiwemo wizi wa miundombinu ya maji taka hasa mifuniko,
wananchi kutupa taka ngumu kwenye mabomba ya maji taka hali inayopelekea
mifereji kuziba na kusababisha kero ya kuvuja kwa maji taka kwenye makazi ya
watu, wananchi kutozingatia matumizi sahihi ya maji safi hali inayopelekea
upotevu wa maji, wanachi kutopenda kusoma taarifa za maji na kusababisha kero
wakati wa kulipa bili, wizi wa maji pamoja na mita.
DUWASA
ina matarajio makubwa kufikia mwaka 2025 ikiwemo kukamilika kwa miradi yote
inayoendelea hivi sasa ili kutimiza lengo la Serikali ya Awamu ya sita kwa
Makao makuu ya nchi kwani Serikali imehamia Dodoma na bado viongozi wanaendelea
kuhamia kwa awamu tofauti hivyo ni lazima miundombinu ya maji iwe ya uhakika na
thabiti ili kuweza pia kuvutia wageni wakiwemo wawekezaji wanaoingia kwa wingi
katika Mkoa huu.
MWISHO
Comments
Post a Comment