TEKNOLOJIA YA MAKINGA MAJI YAZINDULIWA CHEMBA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongela amezindua teknolojia mpya ya kuzuia mmomonyoko wa udongo shambani inayojulikana kama makinga maji iliyobuniwa na TARI - Makutupora kwa kushirikiana na Lead Foundation katika siku ya Mkulima iliyofanyika katika Kijiji cha Mirambo kilichopo Kata ya Goima kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.
Amesema mwongozo huo unatarajiwa kuwasaidia maafisa ugani pamoja na wakulima kudhibiti mmomonyoko shambani kwa kutumia makinga maji aina ya "fanya juu" na upandaji wa mimea pia kusaidia kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji.
Mhe Senyamule amesema"Uzalishaji wa mazao ya kilimo hutegemea utunzaji na uhifadhi bora wa udongo. Mkulima asipozingatia uhifadhi au utunzaji bora wa udongo wakati wa kutumia, huathiri ubora wake katika kuzalisha mazao shambani. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inafanya kazi na wadau mbalimbali katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini na leo tupo hapa kuona na kujifunza kwa vitendo mbinu na teknolojia mbalimbali zinazotumika kuhifadhi udongo na maji shambani katika shamba letu hili la mfano" Amesema Mhe Mongela
Hata hivyo, Afisa Kilimo Bw. Abraham Benard, amewahimiza wananchi wa Mirambo kuweka makinga maji kwenye mashamba yao kwani yanaweza kuwa msaada Mkubwa kwa kilimo Bora na cha Kisasa.
"Kama tunavyoona makinga maji haya yatatusaidia, basi kila mmoja aweke shambani kwake. Fikiria matokeo ya kilimo hiki kwani kinaweza kumtokomeza adui ujinga, umasikini utatatuliwa na shamba na wataalamu wapo. Hakuna wakati tunaohitaji kutumia wataalamu kama kipindi hiki" Amehimiza Bw. Abraham
Vilevile Dkt. Mateete Bekunda ambaye ni Mtafiti kutoka Taasisi za utafiti katika nchi za ki-tropikali (IITA) ambao pia ni wadau na miongoni mwa wagunduzi wa njia hii ya kisasa ya makinga maji amesema kuwa amegundua njia hii kutoka na kushtushwa na hali ya mmomonyoko uliokithiri kwenye mashamba maeneo mengi aliyopita. Ameongeza kuwa, teknolojia zilizowekwa kwenye kitabu hiki, zitumike kwenye Kijiji hiki ili kuendeleza kilimo huku akitoa Rai kwa wakulima kutumia teknolojia hii.
Teknolojia ya makinga maji ambayo inatumia matuta ya kufunga ili kuongeza tija katika uhifadhi wa udongo na maji kwenye Kilimo cha Kisasa, ni njia bora na ya kisasa ambayo kama itatumika ipasavyo hasa kwenye maeneo yenye changamoto ya mmomonyoko wa udongo, itasaidia sana kuinua sekta ya kilimo nchini ambayo bado ndio uti wa mgongo wa Taifa letu. Miongoni mwa wadau walioshiriki katika uzinduzi huo ni Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI), IITA na LEAD FOUNDATION chini ya udhamini wa watu wa Marekani.
MWISHO
Comments
Post a Comment