MACHINGA DODOMA WAMPONGEZA DKT. SAMIA SULUHU HASSAN
Kundi la Machinga Mkoa wa Dodoma
leo tarehe 23/03/2023 wamefanya maandamano ya amani ya kumpongeza Mhe. Dkt
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaheshimisha
ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.
Akipokea maandamano hayo ya amani
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewapongeza wafanyabiashara
wadogowadogo (Machinga) kwa kufanya kazi zao kwa utulivu na juhudi na kutambua
mchango wa Rais Mama Samia Suluhu katika kipindi cha miaka miwili madarakani.
"Ninayo furaha kwasababu
kundi hili ambalo nchi yetu imekuwa ikihangaika nalo leo ni kundi ambalo
linafuraha na amani na linafanya kazi zake kwa utulivu katika mkoa wetu
niwapongeze kwa juhudi, Utashi, busara na hekima na ndio maana leo hii mmeona umuhimu
wa kumpongeza Mhe. Rais wetu.
"Jambo mlilofanya Leo
linaipa fahari Dodoma kama ambavyo risala yenu inasema Mambo yaliyofanyika ni
mengi mno na yataandikwa kwenye historia ya nchi ya Tanzania lakini huenda Afrika
Mashariki kwasababu Machinga Dodoma ni sehemu ya mfano na nyie mmewaona wageni
mbalimbali wakitembelea hapa kufanya utalii."Amesema Senyamule
Kwa upande wake Mwenyekiti
Msaidizi Machinga Mkoa wa Dodoma Bw. Christian Msumari ameishukuru Serikali ya
awamu ya Sita kwa kuwatambua kama kundi rasmi na kuwaweka chini ya Wizara ya Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu jambo ambalo
linawapa urahisi wa kutimiza majukumu yao kwa kusimamiwa na kupatiwa Mafunzo
mbalimbali.
"Tunashukuru kwa kututambua kama
kundi rasmi na kutuweka chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake
na Makundi Maalumu na kwa kufanya hivo imetumefanya tuweze kupata Mafunzo ya
uongozi na tumepata Wizara ya kutulea na kutusaidia.
"Tunamshukuru mama kwa
kutupatia mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji
inayolenga makundi ya vijana, wanawake, walemavu na Machinga tukiwa kundi jipya
lililoongezwa kunufaika na mikopo na sisi tumenufaika nayo kupitia vikundi vya
watu watano na kila aliyekidhi vigezo amepatiwa shillingi milioni 1" Amesema
Bw. Msumari
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini
Mhe. Jabir Shekimweri amewaasa wamachinga wa soko hilo kutunza miundombinu ya
soko hilo ili kuendelea kufanya kazi zao kwa urahihisi na kuhakikisha linadumu kwa
muda mrefu.
Hafla hiyo imeadhimishwa kwa
kaulimbiu ya "miwili ya mama fur-SAMIA kwa wamachinga" huku mgeni
rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule, halfa iliyofanyika
katika soko la Machinga Complex Dodoma na kuandaliwa na wafanyabiashara wenyewe.
Comments
Post a Comment