ZINGATIENI USAFI AWAASA WANANCHI - SENYAMULE
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewaomba
wakazi wa Jiji la Dodoma kuzingatia usafi wa mazingira kila siku ili kuliweka
Jiji katika Hali ya usafi ili kuendelea kuipa hadhi na mvuto wa makao Makuu na
kuepuka magonjwa ya mlipuko.
Senyamule ameyasema hayo alipokagua usafi wa mazingira
katika Kata ya Chamwino Jijini humo uliofanywa na wananchi wa kata hiyo katika
mazingira ya ofisi ya kata hiyo.
"Nitoe wito kwa wanachamwino tuendelee kufanya usafi
siku zote tusiwe tunangoja siku ya Jumamosi ili mji wetu uingie katika miji
Bora sio tu Tanzania bali Duniani. Ninyi wananchi ndio mtakaofanya mji uwe
nadhifu ili kufanikiwa katika hili inatakiwa tusitupe taka hovyo na kuzingatia
kanuni zote za usafi na hifadhi ya mazingira ikiwa ni pamoja na kutoa kwa
wakati taka zinazokusanywa katika miji na kupelekwa dampo" Senyamule
amesisitiza
"Mji wa Dodoma Umepewa baraka ya kuwa makao Makuu ni
lazima kila kitu kiwe kwa mpangilio na kuzingatia viwango vinavyokubalika katika
majiji pia tuendelee kupanda miti ili kukijanisha Dodoma" Amesema
Senyamule
Aidha Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndg.
Dickson Kimaro Amesema hadi sasa wamekusanya zaidi ya shillingi milioni moja
kwa wale wote wasioshiriki katika zoezi Hilo.
" Kwa wananchi ambao hawatekelezi Sheria ya kufanya
usafi Huwa tunawatoza faini na Hadi kufikia hii Leo Zaid ya million moja
imekusanywa Kama faini kwa wale wote wanakutwa wakiendelea na shughuli muda
ambao umetengwa kwa ajili ya usafi",Amesema kimaro
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Mwaja ambapo ndipo
zilipo ofisi za kata Bw. Athumani Makuka amekiri kuwachukulia hatua wale wote
wasiozingatia kanuni na taratibu zilizowekwa katika kutimiza adhma ya kuliweka
Jiji katika Hali ya usafi muda wote.
"Ushiriki wa wananchi ni mzuri na unatia moyo tangu
tulipoanza masuala ya usafi na tumekuwa tukiwaomba Taasisi mbalimbali za
mazingira kushirikiana na sisi na wamekuwa wakituunga mkono katika kulitekeleza
hili.
"Tunawachukulia Sheria wale wote wasio hudhuria siku ya
usafi ambayo ni jumamosi ikiwa ni kutozwa faini na kufikishwa kwenye Ofisi ya
Mtendaji wa kata na tunashirikiana na polisi jamii katika kulitekeleza agizo
hili la usafi wa mazingira na kuliweka Jiji letu katika Hali ya usafi,
"Amesema Makuka
Comments
Post a Comment