SENYAMULE AWAKABIDHI TIKETI ZA KUTALII MWAKINYO NA KUVESA
Mkuu wa Mkoa Dodoma Mhe. Rosemary
Senyamule ametoa tiketi za kufanya utalii katika jijini la Dodoma kwa wachezaji
wa mchezo wa masumbwi bondia Hassan Mwakinyo na Mardochee Kuvesa Katembo raia wa
Afrika kusini mara baada ya pambano lao litakalofanyika kesho tarehe 23/04/2023.
Pambano hilo la kimataifa limeandaliwa na Kampuni ya Lady in Red limelenga kuchangia upatikanaji wa taulo za kike zisizopungua 40,000 ambazo zitawasadia kusoma kwa uhuru na kuweza kutimiza ndoto zao.
Senyamule ameyasema hayo leo tarehe 22/4/2023 alipokutana na mabondia hao na kuwakabidhi tiketi hizo katika Ukumbi wa Mkapa Jijini Dodoma. Senyamule amesema amefurahishwa na pambano kufanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoa Dodoma kwakuwa ni fursa muhimu ya kutangaza utalii na kusisitiza kuwa mabondia hao watatembelea hifadhi mbalimbali ambazo ni Mkungunero, Kolo, Ngorongoro na Tarangire na kutoa rai kwao kuwa mabalozi wazuri nje na ndani ya Mkoa wa Dodoma na Taifa .
"Jambo hili ni kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pia ni fahari kubwa kwa wanadodoma kutuletea mtu maarufu Mwakinyo amekuwa na jina kubwa ndani na nje ya Tanzania nimefurahi leo wanadodoma wanaenda kukuona mubashara katika ukumbi wa nyumbani na sisi tunasema Dodoma ni Fahari ya Watanzania lakini wewe unaenda kuifanya Dodoma ipate iyo Fahari na matumaini yangu wanadodoma wataitumia hii fursa” Senyamule amefafanua
"Sisi tunataka kufanya Mkoa wetu uwe sehemu ya utalii na katika kuendeleza hayo yapo mambo mengi tumeanza kuyafanya moja ni utalii wa mchezo leo tumeanza na mchezo huu wa ngumi siku nyingine ifuate mchezo mbalimbali ili tuweze kupata burudani sasa hili pambano linaenda kudhihilisha utalii nakuonyesha kuunga juhudi za mhe. Rais na baada ya mapambano kumalizika itakua ni sehemu ya kuutangaza mkoa wa Dodoma" Amesisitiza Senyamule
Kwa upande wake Mhe. Sophia Mwakagenda Mbunge wa viti maalumu ambaye ndio mwandaaji wa pambano hilo amesema kuwa tukio hili limelenga kukusanya fedha kwa ajili ya kukusanya taulo za kike ili kuwasaidia wototo hao kwani ni sehemu ya kusimamia haki zao za msingi za kupata mafunzo wakati wote. Aidha, amempongeza Bondia Hassan Mwakinyo kwa kukubali kujitoa katika kushiriki pambano ili kuwasaidia watoto wa kike.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Senga Gugu amesema kuwa pambano hilo litakuwa ni kubwa na la kimataifa hivyo amewataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kushuhudia mapambano hayo.
Kwa upande wake Bondia Hassan Mwakinyo ambaye ni mshiriki wa pambano hilo amesema amefurahishwa na waandaji wa pambano hilo kwani litasaidia kuwapatia watoto wa kike kupata taulo hali ambayo itawafanya kusoma kwa amani kipindi wanapokua darasani na kutopoteza masomo yao na kutimiza ndoto zao.
Amewashukuru pia Wizara ya Maliasili
na Utalii na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuona kuna fursa na kutumia wanamchezo
kwani ni sehemu nzuri ya kulitangaza jiji la Dodoma na Taifa .
Aidha Mhe.Senyamule ameshuhudia zoezi upimwaji wa uzito na afya kwa mabondia wote wawili lililofanyika katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma ambapo ni rasmi pambano hilo litapigwa kutokana na mabondia hao kuwa na uzito unaolingana.
Comments
Post a Comment