TBS YATOA VYETI 29 VYA UBORA KANDA YA KATI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Senga Gugu amewatunuku Vyeti na Leseni wafanyabiashara na wazalishaji ambao bidhaa zao zimethibitishwa Ubora wake na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa wazalishaji wa kanda ya kati (Dodoma, singida na Tabora) pamoja na Iringa na kuwaasa wazalishaji kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa viwandani zinazingatia kanuni bora za uzalishaji.
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe Aprili 28,2023 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
"Kazi
hii iliyofanywa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kupitia TBS ni
mwendelezo wa azma ya Serikali katika kuhakikisha wazalishaji wa bidhaa
viwandani kama wadau muhimu wa maendeleo ya ubora na usalama wa bidhaa, wanazalisha
bidhaa zinazokidhi matakwa ya Viwango vya ubora Kitaifa na kimataifa na
kuhakikisha Watanzania wananunua na kutumia bidhaa zenye ubora na ambazo
ni salama kwa afya zao na mazingira
"Nitoe rai kwenu nyote ambao mmeshiriki kutimiza wajibu wenu kwa kuweka uzalendo mbele kwa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kusambazwa nchini ni bora na salama. Sambamba na hilo niwaagize muendelee kuwa mabalozi wazuri kwa wazalishaji wengine ambao bado hawajathibitisha ubora wa bidhaa zao, lengo likiwa ni kuwa na soko lenye bidhaa bora kwa matumizi ya ndani na nje ya Tanzania, ninaamini kuwa hafla hii ni njia mojawapo ya kuleta tija katika udhibiti wa bidhaa ndani ya Mkoa wetu, Kanda na Taifa kwa ujumla "amefafanua Gugu
Naye, Meneja wa Kanda ya Kati Bw. Nikonia Mwabuka ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania amesema wazalishaji kuendelea kuwa waaminifu na kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na Shirika la Viwango ili bidhaa ikithibitishwa ubora ni kuhakikisha kuwa afya za wananchi na mazingira zinalindwa kwa kila mmoja .
"Bidhaa ikithibitishwa ubora wake na nchi wanachama ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki bidhaa hiyo itaingia katika nchi wanachama pasipo kukaguliwa na kupimwa tena ili kutambua ubora wake ." Amesema Mabuka
Jumla
ya Vyeti na Leseni 29 za wafanyabiashara na wazalishaji zimetolewa na
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa wazalishaji wa kanda ya kati (Dodoma,
singida na Tabora) pamoja na Iringa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment