GWAJIMA AZINDUA PROGRAM YA JINSIA YA INTERNATIONAL FINANCE CORPORATION {IFC}











 


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothh Gwajima amezindua Programu ya Jinsia ya ANAWEZA itakayowawezesha wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango leo Mei 31, 2023.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Gwajima amesema Programu hiyo itakayogharimu fedha za Kimarekani milioni 7.5 inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 , Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050, Sera ya Maendeleo na Jinsia ya 2000 na Sera ya Jinsia ya 2016 ya Zanzibar.

"Uzinduzi wa Programu ya ANAWEZA ambayo inalenga kumkomboa mwanamke kiuchumi, imekuja kwa wakati muafaka ambapo Tanzania ipo katika jitihada za kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi. Tanzania ni mojawapo ya Mataifa yanayotekeleza malengo ya Jukwaa la Kimataifa ya Kukuza usawa wa Kijinsia. Katika hili Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kinara wa utekelezaji wa Jukwaa hili hususan kuhusu Haki na Usawa wa Kiuchumi" Amesisitiza Dkt. Gwajima

Waziri Gwajima ameongeza pia, pamoja na kuwa Wanawake ni tegemeo kubwa katika Taifa, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mila na destruri zenye madhara, elimu duni, ukosefu wa mitaji na stadi za ujasiriamali ambapo Serikali imechukua hatua ya kuboresha kipato na kuondoa umaskini kwa wanawake na wanaume nchini.

Amezitaja baadhi ya hatua hizo, kuwa ni pamoja na fursa za mikopo ikiwemo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mikopo ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake na kupitia madirisha mahsusi kwenye Benki mbalimbali.

Amesema hatua nyingine ni uanzishwaji wa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mikoa yote Tanzania Katika ambapo wanawake wameendelea kupata taarifa na fusa za kiuchumi.

Aidha, Dkt. Gwajima amebainisha kwamba programu hiyo inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na Sekta binafsi lengo ni ifikiapo mwaka 2026 hali ya Wanawake iwe imebadilika kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Riziki Pembe amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa wanawake kutokana na uwezo walionao katika uongozi kwenye nyanja

Naye ,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema umefika wakati wanawake wanatakiwa kuthubutu wenyewe bila kusukumwa kwa kujitambua na kuamka wenyewe yani kujenga kujiamini wenyewe.

" Leo tunashuhudia juhudi za Serikali za kuhakikisha mwanamke anapata haki sawa katika sekta zote, naamini kupitia mradi huu wanawake wengi watapiga hatua za kiuchumi, kijamii na hasa kutumia nafasi hii vizuri kuweza kupata nafasi za uongozi mbalimbali ili kuweza kufikia wanawake wengi zaidi wa ngazi zote" amefafanua Senyamule

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri ATE Sussane Ndomba ambapo Programu hiyo itatekelezwa chini ya Chama hicho, amebainisha kwamba Chama hicho kinajali usawa wa kijinsia hasa mahala pa kazi na tangu mwaka 2016 chama hicho kimekuwa na programu ya mafunzo kwa wanawake 274 hadi sasa.

Akieleza lengo la mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka 5, Mkurugenzi wa Shirika la Fedha la Kimataifa IFC Kanda ya Afrika Mashariki Jumoke Jagun Dokunmu amesema usawa wa kijinsia utafikiwa iwapo kutakuwa na usawa wa kiuchumi kati ya wanawake na wanaume, ili wanawake waweze kushiriki vema nafasi za uongozi.


MWISHO.

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WA HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA WATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

‘WANAWAKE NA SAMIA’ 3000 MKOA WA DODOMA KUPATA MAFUNZO VETA