SENYAMULE AAGIZA UJENZI WA MADARASA KUKAMILIKA KWA WAKATI
Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo Mei 29, 2023 ameendelea na ziara ya
kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni katika Shule ya wasichana Bunge,
ujenzi wa Shule mpya ya msingi katika eneo la Swaswa na madarasa ya awali
katika Shule ya msingi Kisasa ambapo ujenzi wake uko katika hatua za ukamilishaji.
Katika
kaguzi hizo Mhe. Senyamule ametoa maagizo kwa wasimamizi wa mradi kuhakikisha
kazi inakamilika kwa muda uliopangwa na kuzingatia viwango vya ubora huku
akitoa rai kwa wasimamizi wa ujenzi kukaa na mafundi ili kufanikisha
ukamilishaji wake.
“Mkoa wa
Dodoma tumejipanga kukamilisha hizi kazi kwa wakati hivyo wataalamu mkae na
mafundi mpitie kwa pamoja mpango kazi wa miradi hii ili tujue kila siku ni kazi
gani inatakiwa kukamilika kwa siku husika ili itakapofika tarehe 15 Juni 2023
ujenzi uwe umekamilika” Senyamule amesisitiza.
Aidha, Senyamule
amesema kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ametoa fedha zote kwa wakati hivyo hakuna sababu za kuchelewa kufanya manunuzi.
Amesema ni wajibu wa wataalamu kuhakikisha ununuzi wa vifaa vyote vinavyohitajika
vinapatikana ili mradi uweze kukamilika kwa muda uliopangwa.
Mkoa wa
Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa
ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madasa ya msingi 163, madarasa ya awali
16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu.
Shule ya
Msingi Kisasa imepokea kiasi cha Shilingi Milioni 63.6 kwa ajili ya ujenzi wa
madarasa 2 na vyoo 6 huku Shule ya Swaswa imepokea kiasi cha Shilingi Milioni 318.8
kwa ajili ya kujenga Shule mpya itakayokuwa na madarasa ya msingi 7, madarasa
ya awali 2 na Vyoo 12.
MWISHO
Comments
Post a Comment