EAST AFRICA BICYCLE TOUR' WAAGWA DODOMA
Waendesha baiskeli wanaozunguka nchi za Afrika Mashariki ambao waliwasili jana Mkoa wa Dodoma nchini Tanzania, wameagwa rasmi leo Agosti 29 na uongozi wa Mkoa ili kuendelea na safari yao kuelekea nchini Burundi.
Akiwaaga waendesha baiskeli hao, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bi. Coletha Kiwale, amewapongeza na kuwasisitiza kuimarisha umoja.
"Hongereni kwa kupumzika Dodoma. Nimefurahi kuanzisha Tour kama hii ambayo inawakutanisha wote wana Afrika Mashariki, inaimarisha amani na umoja hivyo tunatakiwa kuendeleza utaratibu huu. Tunashukuru pia kwa ajenda yenu ya utunzaji wa mazingira kwani Dunia nzima sasa inahamasisha hilo. Nawaomba muendelee kuimarisha umoja huu" Amesema Bi. Kiwale.
Aidha, waendesha baiskeli hao wameshukuru kwa mapokezi mazuri waliyoyapata kwenye Mkoa wa Dodoma na wameahidi kuendelea kusambaza amani na kusafisha mazingira hasa kwa kuwafundisha watoto umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Safari ya waendesha baiskeli hao ilianzia katika Jiji la Kampala nchini Uganda, ikafika nchini Kenya na Sasa ni Tanzania na kutoka hapa wanaelekea nchini Burundi na wanatarajia kutumia siku 58 kutamatisha safari nzima ya kuzunguka nchi za Afrika Mashariki. Serikali ya Mkoa wa Dodoma inawatakia safari njema.
MWISHO
Comments
Post a Comment