MRADI WA KOFFIH WAIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI NA MTOTO
Idara ya Afya chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma imefanya kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto kilichofunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule ambaye amewakilishwa na Katibu Tawala Mkoa Bw. Ally Gugu katika Hoteli ya Vizano Jijini Dodoma.
Mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri mbili za Mkoa wa Dodoma ambazo ni Kongwa na Mpwapwa chini ya udhamini wa Taasisi ya nchini Korea inayojulikana kama KOREA FOUNDATION FOR INTERNATIONAL HEALTH CARE (KOFIH) ambapo wadau mbalimbali wa afya kutoka katika Halmashauri hizo wamehudhuria kikao hicho.
Akifungua kikao hicho Bw. Gugu amesema tafiti zilizofanywa na Tanzania Demographic Health Survey ya mwaka 2022, inaonyesha viashiria vya huduma ya afya ya uzazi kwa Dodoma inafanya vizuri. Pia ameainisha idadi ya vituo vinavyotoa huduma ya afya kwa Mkoa wa Dodoma ambavyo vimekua chachu ya utoaji wa huduma Bora za afya.
"Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Dodoma una vituo vya afya 542 ikiwa ni pamoja na Hospitali 16, vituo vya afya 69, Zahanati 436 na kliniki maalumu ( Polyclinics) 21. Kati ya vituo hivyo, vituo 410 sawa na asilimia 76 vinatoa huduma za afya ya uzazi na Mtoto na vituo 23 sawa na asilimia 39 kati ya vituo vya afya 59 vya umma vinatoa huduma za dharura za upasuaji kwa Mama wajawazito" Amebainisha Bw. Gugu.
Aidha, katika taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Huduma za afya ya uzazi na Mtoto Mkoa wa Dodoma Bi. Nice Moshi imesema kuwa KOFIH imetekeleza mradi wa huduma ya afya ya uzazi na Mtoto ambao ni wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 katika Halmashauri za Kongwa na Mpwapwa ambapo tathmini hii ni ya miaka miwili.
" Katika kipindi hiki cha miaka miwili, Halmashauri za Kongwa na Mpwapwa zimenufaika na uboreshwaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto ambao ndio lengo kuu la mradi huu. KOFIH pia imesaidia kukarabati vituo sita vinavyotoa huduma za upasuaji katika Halmashauri hizi pia utolewaji wa huduma za Elimu ya afya ya uzazi kwa jamii na mashuleni imeimarika kwa kiasi kikubwa" Amesema Bi. Moshi
Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kitengo cha afya na lishe Dkt. Mageda Luhulya, ameelezea faida za mradi huu kwa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma kwa ujumla kwa kusema kuwa mradi huu umekua na faida nyingi ikiwemo kuhusisha mpango wa damu salama, ujenzi na ukarabati wa vituo vya huduma za afya na ununuzi wa vifaa tiba. Pia ameongeza kuwa Tanzania imekua na mabadiliko makubwa katika sekta ya afya kwa sasa na kupelekea vifo vya mama mjamzito na Mtoto kupungua kwa kasi. Serikali na KOFIH zimeshirikiana kumaliza kabisa tatizo hili siku za mbeleni.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Dkt. Thomas Mchomvu, ameelezea utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri yake.
"Mradi unatekelezwa kwenye vituo vya afya vya Chamkoroma, Mkoka na Kibaigwa ambapo Halmashauri imefaidika na ongezeko la ukusanyaji wa damu salama kufikia uniti 977 sawa na asilimia 146 kutoka uniti 166zilizotarajiwa, mwamko wa Elimu ya afya ya uzazi katika jamii umekua mkubwa kwa kupelekea viongozi 300 wa jamii mbalimbali na Wanawake 900 kupatiwa Elimu ya afya, Elimu ya uzazi imeweza kufikishwa mashuleni ambapo jumla ya shule 20 ikiwemo 10 za msingi na 10 za sekondari zimefikiwa katika Halmashauri hii" Dkt. Mchomvu.
MWISHO
Comments
Post a Comment