DODOMA KUTUMIA GESI ASILIA MAJUMBANI











 Uongozi wa Kampuni  inayojishughulisha na usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo viwandani, usafirishaji na majumbani kutoka nchini Japan (JIKA), leo Oktoba 30, 2023, imekutana na uongozi wa Mkoa wa Dodoma chini ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Rosemary Senyamule kujadili mpango wa kusambaza gesi asilia ndani ya Mkoa wa Dodoma ikiwa ni miongoni mwa mikoa mitatu iliyochaguliwa ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma na Pwani.


Akifafanua sababu za kuichagua Dodoma kuwa moja kati ya mikoa itakayofanikisha mpango huo, Msimamizi wa Mradi wa gesi asilia kutoka JICA Bw. Shinji Omoteyama amesema Dodoma ni Mji ambao hauna msongamano mkubwa hivyo ni salama kwa upitishaji wa mabomba ya gesi yatakayochimbiwa ardhini. 

Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule, ameipongeza JICA kwa kuichagua Dodoma kwani kwa Sasa ndio Mkoa unaokua na kujengeka kwa kasi huku miradi mbalimbali ya kimkakati ikitekelezwa.

"Dodoma inahitaji maendeleo mapya kwani ni Mji mpya unaokua kwa kasi kimaendeleo kutokana na ujenzi wa miradi mbalimbali kama vile kiwanja cha ndege cha Msalato, barabara za mzunguko wa nje (outer ringroad) na mingine mingi hivyo, uhitaji wa matumizi ya gesi ni mkubwa. Mkoa wa Dodoma una ramani ya mipango miji inayoainisha maeneo ya viwanda, makazi na miundombinu mbinu mingine. Ramani hiyo huwa inafanyiwa marekebisho kila baada ya miaka mitano na kwa mara ya mwisho marekebisho yalifanyika mwaka 2019 ambayo yalitaka kuwepo kwa kituo cha kusambazia gesi asilia ndani ya Mkoa" Amesema Mhe Senyamule 

Naye Mkurungenzi wa Mradi kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Joyce Kisamo, amesema mpango wa kusambaza gesi asilia kwa Mkoa huo ulianza tangu mwaka 2022 ukisimamiwa na Kampuni ya JICA na uliandaa usanifu kwa mikoa hiyo mitatu kwa ahadi ya kuongeza  mingine zaidi hapo baadae. Ametaja matumizi ya gesi asilia kuwa itatumika kwa matumizi ya nyumbani (kupikia) kwa kuunganisha mabomba kuelekea kwenye makazi ya watu na kwenye vyombo vya moto hivyo kuwa mbadala wa mafuta ya petroli.

Maeneo yaliyochaguliwa kwa ajili ya Mradi huo ni Mji wa Serikali (Mtumba), Iyumbu pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA