MRADI WA BARABARA YA MACHINGA WAKABIDHIWA KWA MKANDARASI
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Machinga complex yenye urefu wa Km 0.65 kwa
kiwango cha lami, umekabidhiwa kwa mkandarasi Oktoba 30, 2023. Hafla hiyo ya
makabidhiano imehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule
akiwa ndiye mgeni rasmi kwenye viwanja vya soko la Machinga Jijini Dodoma.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dodoma Injinia Edward Lemelo, ametoa ufafanuzi
wa namna utekelezaji wa Mradi huo utakavyofanyika.
"Ujenzi wa Machinga complex umesainiwa tarehe 25 Oktoba kwa shilingi
1,034,876,565.55 na Mkandarasi Nyanza Road Works Limited wa Dodoma kwa kipindi
cha siku 180. Leo hii tupo hapa kwa ajili ya kumkabidhi eneo la mradi tayari
kwa kuanza kazi. Kukamilika kwa matengenezo haya, kutarahisisha uingizwaji wa
bidhaa sokoni na pia kutaboresha mazingira ya soko letu. Ujenzi huu utaambatana
na ujenzi wa kitako cha barabara Km 0.65, matabaka manne ya barabara yaani G7,
G15, C1 na CRR, uwekezaji tabaka la juu kwa lami ngumu yaani Asphalt Concrete
Km 0.65, mitaro ya maji ya mvua Mita 1300 pande zote za barabara, uwekaji wa
taa 20 za barabarani na njia za watembea kwa miguu" Amesema Injinia
Lemelo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule, amesema kuwa makabidhiano ya
barabara hii kwa mkandarasi ni mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi za ujenzi wa
soko la Machinga zilizotolewa mwaka 2022 na amewausia kutunza mazingira ya eneo
hili ili miradi idumu.
"Leo ni mwendelezo wa ahadi za Serikali kwenye soko hili, ikiwemo lami,
uwekaji taa za barabarani na njia ya watembea kwa miguu zinawekwa kwa pamoja
hivyo mkandarasi hakikisha unaharakisha ujenzi wa barabara hii uweze kukamilika
nyuma ya wakati ili machinga waweze kufanya kazi zao saa 24. Pia natoka Wito
kwenu mupande miti kwenye eneo hili kwani ni la wazi na litawezesha utunzaji wa
mazingira kwani eneo hili linatembelewa na watu wengi kwa lengo la kujifunza
kupitia mradi huu hivyo uzuri wa miundombinu hii utadumu endapo itatunzwa
vizuri kwa kufanyika usafi" Mhe. Senyamule.
Vilevile, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe Jabir Shekimweri, ametoa rai kwa
wananchi na Taasisi zinazohusika na upitishaji wa miundombinu yake kushirikiana
na Mkandarasi kufanya tathmini ya njia za miundombinu yao ili kuzuia uharibifu
pindi mradi unapokamilika. Pia amewataka wananchi kushirikiana na Mkandarasi
wakati wa utekelezaji wa Mradi na wakati wa maudhi madogo madogo
yatakayosababishwa na utekelezaji wa Mradi yatakapojitokeza.
Utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa barabara ya Machinga complex kwa kiwango cha
lami unatekelezwa na Mkandarasi ajulikanaye kama Nyanza Road Works Limited
chini ya Mhandisi Msimamizi ambaye ni Meneja wa TARURA Wilaya ya Dodoma. Mradi
huu unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 6 (siku 180).
MWISHO
Comments
Post a Comment