KONGWA AFRICAN LIBERATION MARATHON YAFANA.










Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel amesema mashindano ya 'Kongwa African Liberation Marathon' yana lengo la kuwakumbusha Watanzania namna Tanzania kupitia Wilaya ya Kongwa ilivyoshiriki katika kupigania Uhuru wa Mataifa Mengine ya Afrika.

Ni katika viwanja vya Saba Saba Halmashauri ya Kongwa leo Novemba 25/2023 kulipofanyika mbio hizo ambapo Mhe. Mwema ameweka bayana dhamira ya kuanzishwa kwa mbio hizo ni kuukumbusha Umma wa Watanzania namna Wilaya yake ilivyoshiriki katika kupigania Uhuru wa baadhi ya Mataifa ya kusini mwa Afrika.

"Tunachokifanya leo ni kuwakumbusha Watanzania ili watambue kuwa nchi Yetu hususan Mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Kongwa, ilisaidia kwa kiasi kikubwa kupigania Uhuru wa baadhi ya Nchi za kusini mwa Afrika kupitia Kambi ya mafunzo ya wapigania Uhuru ambayo ilikuwa hapa Kongwa," Mhe. Mwema

Hata hivyo, Mhe. Mwema amebainisha kuwa mbio hizo za 'Kongwa African Liberation Marathon' zitaendelea kufanyika Kila mwaka huku wakiongeza wigo mpana kwa kuwashirikisha Mataifa mbalimbali ya Afrika.

"Tutaendelea kufanya  muendelezo wa mbio hizi mwaka 2024 na Miaka ijayo lakini mwakani tumepanga kuzifanya kwa upana wa kuyashirikisha Mataifa mbalimbali ambayo viongozi wake waliweka Kambi ya kupatiwa mafunzo hapa na baadhi yao walikuja Kongwa kujificha katika Mahandaki yanayopatikana hapa," Mhe. Mwema

Mkuu huyo ameyataja Mataifa ambayo viongozi wake wapigania Uhuru walifika Kongwa na kuweka Kambi ya muda kuwa ni pamoja na Msumbiji, Afrika kusini, Namibia, Angola, Zambia na Zimbabwe.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongela, akisoma Hotuba kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali kupitia Wizara hiyo imetenga Fedha maalum kwaajili ya ukarabati wa mahandaki yaliyotumiwa na viongozi wa Nchi kusini mwa Afrika.

"Nimefurahishwa kwamba mwaka wa Fedha 2023/24 Wizara kupitia kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika imetenga Fedha maalum ya kufanya ukarabati wa Mahandaki yaliyotumiwa na viongozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika likiwemo Handaki lililotumiwa na Hayati Samora Machel wakati alipojihami na hatari", Amesema Dkt. Ndumbaro

Mbio hizo zilizoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Kongwa pamoja na wadau mbalimbali, zimefanyika hii leo huku zikiwajumuisha  wakimbiaji wa mbio za 5km, 10km na 21km na washindi wamepatiwa zawadi za Fedha taslimu pamoja na Medali za pongezi kwa kushiriki na kumaliza mbio hizo.

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA