NZUGUNI KUNUFAIKA NA MRADI MKUBWA WA MAJI.
Wananchi na wakazi wa Eneo la Nzuguni wanaelekea kupata afueni ya changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa maji baada ya kukamilika kwa mradi Mkubwa wa Maji unaotekelezwa kwa fedha za Serikali kiasi cha Shilingi Bilioni 4.8 unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi Januari 2024. Mradi huo una lengo la kuongeza kiasi cha maji yanayosambazwa kwa wananchi kwa asilimia 11.7
Hayo yamebainishwa leo Novemba 27, 2023 wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipotembelea mradi huo wa maji kujionea hatua iliyofikiwa. Mhe. Senyamule ameshuhudia ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhia na kusambazia maji lenye ujazo wa Lita Milioni 3 likiwa na urefu wa mita 300 pamoja na uchimbaji wa visima virefu Hadi mita 300 kwenda chini ya ardhi.
"Leo tunashuhudia matokeo ya Matumaini yetu ya siku nyingi ya kuwa siku moja tutapata maji kwenye eneo hili na maeneo ya jirani. Nilikua natamani sana maji yapatikane Dodoma kwa hadhi ya makao makuu. Jambo hili limekua la kihistoria kwa Dodoma. Wananchi, tuendelee kuweka Imani kwa Serikali yetu kwani Ina Imani kubwa ya kumaliza tatizo la maji kwa Dodoma.
"Nitoe shime kwa wananchi, muwe na matumizi sahihi ya maji yanayoendana na utunzaji wa mazingira. Maji haya yatumike kwa matumizi ya nyumbani na kumwagilia miti pia kwani tunaendelea na mkakati wetu maalumu wa upandaji miti mitano kwa kila kaya" Amesisitiza Mhe. Senyamule.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri, amemshukuru Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye miradi mikubwa Jijini Dodoma ikiwemo Mradi huo kwani kumekuwa na changamoto ya Maji katika Jiji hilo la Makao makuu ya Serikali ya Tanzania.
Amesema mradi huo uelekeze matumizi kwa wananchi na pia kama inavyofanyika katika utekelezaji wa miradi ya maji safi basi pia ifanyike kwenye miradi ya maji taka ili kuwaondolea adha wananchi katika makazi na maeneo yao.
Kadhalika, akitoa Maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mkurungenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph, amesema hadi Sasa mradi wa ujenzi wa tanki kubwa la ujazo wa Lita Milioni 3.5, umefikia asilimia 96 ukiwa na gharama ya Shilingi Bilioni 4.3 za Kitanzania
Mradi huo unaotarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 75,998 ambao kwa Sasa Umeanza awamu ya pili ya uchimbaji wa visima Vitano na hapo baadae vitaongezwa vingine 11 na unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wa Nzuguni A na B, Ilazo, Kisasa, Nyumba 300, Mahomanyika, Mwangaza na maeneo jirani ya Mradi.
ReplyForward |
Comments
Post a Comment