KONGWA KUNUFAIKA NA MABINGWA WA MACHO
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametembelea na kuzindua kambi ya madaktari Bingwa wa macho inayofanyika katika hospitali ya Wilaya ya kongwa, ambapo dhamira kuu ya kuwepo kwa kambi hiyo ni kuwasaidia wananchi kujua hali za kiafya za macho yao na hizo zinatolewa pasi na gharama zozote.
Mhe. Senyamule amesema kuwa Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa Mikoa
inayotekeleza mradi wa Macho Yangu unaotekelezwa na shirika lisilo la
kiserikali la` Sightsavers` linalojishughulisha na utoaji wa huduma za macho.
“Shirika hili linajishughulisha na utoaji wa huduma za macho
ikiwepo upimaji wa miwani, pamoja na hayo shirika litasomesha madktari
wasaidizi wa macho wawili na wauguzi sita pia litanunua baadhi ya vifaa vya macho
na kusaidia kuundwa kwa mabaraza ya watu wenye ulemavu na kuwezesha huduma za
kliniki tembezi za macho kama hii iliyozinduliwa leo,’’ Mhe. Senyamule
Hatahivyo licha ya manufaa yanayopatikana kutokana na uwepo
wa madaktari hao Mhe. Senyamule amesema miongoni mwa changamoto zinazojitokeza katika
utolewaji wa matibabu hayo ni pamoja na baadhi ya wagonjwa kutofika katika
vituo vya huduma mapema hali inayopelekea baadhi yao kupoteza uwezo wa kuona.
“Pamoja na jitihada zinazofanyika bado kuna changamoto
inayotokana na baadhi ya wagonjwa kushindwa kufika katika vituo vya kutolea
huduma mapema hadi pale wanaposhindwa kuona kabisa, Mradi huu umekuja kwa
wakati na ni matumaini yangu kuwa huduma hizi za kibingwa zitwanufaisha
wananchi wengi,” amesisitiza Senyamule
Kambi ya madaktari bingwa wa macho katika halmashauri ya
kongwa itadumu kwa takribani siku nne kuanzia Disemba 11 -14/12/2023 huku
wananchi wakipatiwa matibabu ya macho bila kuchangia gharama zozote hali
inayopelekea wananchi na wakazi wa Wilaya ya kongwa kunufaika na ujio wa
mabingwa hao.
Comments
Post a Comment