TIMU YA ITIFAKI YATAKIWA KUTAMBUKIWA NA VIONGOZI WAO
TIMU YA ITIFAKI YATAKIWA KUTAMBULIWA NA VIONGOZI WA
Vijana wanaosimamia Itifaki kwenye dhifa
mbalimbali za Kiserikali na hata za Taasisi binafsi wametakiwa kujitambulisha
kwenye ofisi zao ili waweze kutambulika na kutumika kwa ajili ya kusimamia
taratibu na ustaarabu wakati wa shughuli tofauti tofauti zinazotekelezwa Mkoa
wa Dodoma na Mikoa mingine pia pindi huduma yao inapohitajika.
Hayo yameelezwa Leo Desemba 15, 2023 na Mhe.
Rosemary Senyamule wakati akifungua mafunzo siku tatu yanayotolewa kwa timu ya
huduma ya Itifaki yanayofanyika kwenye ukumbi wa Chuo kikuu cha Mipango
kilichopo Jijini Dodoma.
"Nimetiwa Moyo na vijana hawa kwa kuweza
kuhudhuria mafunzo haya. Dodoma ikiwa ndio makao makuu ya nchi, Kuna takribani
ofisi 100 za Serikali hapa hali inayopelekea kuwa na matukio mengi yenye
uhitaji wa huduma hii. Kumekua na changamoto kwenye suala la usimamizi wa
Itifaki kwenye dhifa mbalimbali.
"Mafunzo haya yatawasaidia huko muendapo na
nitoe Wito kwenu, baada ya mafunzo haya, mukajitambulishe kwenye ofisi zenu ili
mukihitajika muweze kutumika. Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anahimiza
kufanyika mikutano mbalimbali hali inayopelekea kuhitajika watu wenye sifa kama
zenu. Mafunzo yenu yatakua na faida kubwa kwa Dodoma" Amesema Mhe.
Senyamule.
Awali akitoa hotuba fupi ya Timu hii, Mwenyekiti
wake Bw. Hussein Aboubakar Hussein, amesema vijana hawa wanashauku kubwa ya
kufanya maendeleo kwenye sekta ya kilimo hivyo ametoa ombi kwa Mhe. Mkuu wa
Mkoa kupatiwa shamba la Hekari 50 na Mhe. Senyamule ameridhia ombi hilo na
kuahidi kuwapatia kwa kuzingatia Mradi mkubwa wa Serikali wa BBT ulioanzishwa
na Wizara ya Kilimo unaolenga vijana kujikita kwenye uwekezaji wa kilimo.
Pia timu hii imepata mafanikio kadhaa ikiwemo
kutambulika na Mamlaka mbalimbali, kusimamia na kushiriki Itifaki wakati wa
mbio za Mwenge, kupata usajili wa Kiserikali pamoja na kuandaa mradi wa
kuwezesha watoto kwenda shule inayotarajiwa kuwa msaada kwa watoto ambao
wanahitaji kwenda shule lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Timu ya Itifaki imesajiliwa tarehe 13 Machi 2023
kwa lengo kuu la kutoa huduma za kiitifaki na uendeshaji wa mikutano na dhifa
mbalimbali ina washiriki 81 wakiwemo Maafisa Itifaki kutoka sehemu mbalimbali,
waajiriwa na wasio waajiriwa kutoka Mikoa tofauti tofauti nchini.
Comments
Post a Comment