DCT NA NEEMA YA MILLIONI 32.8 MWITIKILA-BAHI
Vifaa vya Shule vyenye thamani ya Tsh.Millioni 32.8 vimekabidhiwa
katika Shule za Msingi Mwitikira, Lupeta Mwitikira B na Shule ya Sekondari
Mwitikira kwa ufadhili wa Kanisa la St. Pauls Richmond kutoka Marekani kwa
kushirikiana na kanisa la Anglican Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), ambapo
makabidhiano hayo yamefanyika April 17, 2024 katika viwanja vya kanisa la
Anglican Parish ya Mwitikila Wilayani Bahi.
Vifaa hivyo ni madawati 290, meza 13, Viti 113 na Mashine ya kuchapia na kutolea kopi (printer
machine) vimekabidhiwa na Askofu wa DCT Dickson Daud Chilongani kwa kaimu Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Mayeka S. Mayeka
ambaye amewakabidhi uongozi wa Halmashauri ya Bahi na Uongozi wa Shule hizo.
Akizungumza katika Hafla hiyo Mhe.Mayeka amewataka wakazi wa
kata ya Mwitikira kuacha tabia ya kuwaachisha Watoto wao shule na kuwapeleka
katika majiji mbalimbali kwa lengo la kufanya kazi za ndani zisizo na maslahi
katika Maisha ya Watoto hao.
“Kuna mawakala wanaobeba Watoto vijijini nikuombe OCD na timu yako tuwasake hawa
mawakala ambao kazi yao ni kutembea kutafuta mabinti wawasafirishe kwenye miji
mbalimbali kufanya kazi za ndani, hawa ni watu wabaya kabisa watoto wenu
wanakumbana na unyanyasaji mkubwa wa kijinsia huko mnakowapeleka wakafanye kazi
hawawezi kusema ni siri yao acheni mara moja tabia hii,” ameagiza Mayeka
Aidha Mhe. Mayeka amewaomba uongozi wa kanisa hilo kuendelea
kuunga Mkono juhudi za Serikali kwa kutokukata tamaa ya kujitolea vitu
mbalimbali ambavyo vinagusa Maisha ya Watanzania hususan katika Sekta ya Elimu.
Naye Askofu Chilongani ameahidi kuendelea kushirikiana na
Serikali katika Sekta ya Elimu kwa kuweka bayana kuwa Kanisa hilo limewagharamia
zaidi ya watu 7000 kwa ngazi zote za Elimu pasi na kubagua Imani za Dini za
watu hao.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashari ya Wilaya ya
Bahi Bi. Zaina Mlawa amewapongeza DCT na kukiri kuwa misaada wanayoitoa imekuwa
chachu ya kuongeza ufaulu kwa Shule za kata hiyo ikiwemo Shule ya Sekondari
Mwitikila.
Comments
Post a Comment