WENYEVITI WA BODI NA KAMATI ZA SHULE WATAKIWA KUZUIA UTOVU WA NIDHAMU
Wenyeviti wa bodi na kamati za shule za Msingi na Sekondari Mkoa wa Dodoma, wametakiwa kusimamia nidhamu kwa wanafunzi kwani matukio mengi ya ukiukwaji wa nidhamu yanapotokea huchukuliwa hatua kuliko jitihada za kuzuia yasitokee.
Hayo yamebainishwa leo Mei 17, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wakati wa kikao kazi kilichoitishwa na seksheni ya Elimu Mkoa kwa lengo la kuwajengea uelewa viongozi hao. Kikao hicho kimefanyika kwenye Shule ya Msingi Mtemi Mazengo Jijini Dodoma.
Akifungua kikao hicho, Mhe. Senyamule amesema; "Nafahamu jukumu lenu kubwa ni kusimamia nidhamu, lakini hebu muje na mikakati thabiti ya kuzuia tusipate matokeo ya utovu wa nidhamu. Lazima tutumie nguvu nyingi kulinda nidhamu kabla hatujachukua hatua pale inapovunjwa". Amesema Mhe. Senyamule.
Hata hivyo, Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma Mwl. Vicent Kayombo, amesema kikao hiki ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Mkoa ambayo yamelenga kutimiza Mkakati wa Elimu 2024 uliowekwa kwa shabaha ya kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kwenye mitihani ya Taifa.
"Kikao hiki kimelenga wenyeviti wa bodi na kamati za shule kwa kuwa wao ndio wasimamizi wakuu wa maadili na nidhamu shuleni. Pia lengo la kikao ni kuwajengea uelewa wa pamoja katika kutekeleza Mkakati wa Elimu wa Mkoa.
Mkoa wa Dodoma una jumla ya shule za Msingi 915 na wanafunzi 674,291, shule za Sekondari 251 na wanafunzi 151,363 pamoja na vyuo vya ualimu vitatu (3). Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2024, asilimia 30 ya wananchi wa Dodoma ni wanafunzi hivyo juhudi zinahitajika kulijengea maadili mema kundi hili.
Comments
Post a Comment