BODABODA WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI JUU YA ABIRIA WAO









Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa angalizo kwa  Maafisa usafirishaji wa Pikipiki (bodaboda)  kuchukua tahadhari juu ya abiria wanaowapakia kutokana kuibuka kwa matukio ya kihalifu yanayofanywa na watu wasiojulikana dhidi ya Maafisa hao siku za hivi karibuni.

Rai hiyo imetolewa Juni 18, 2024 wakati wa muendelezo wa utekelezaji wa kauli mbiu "kero yako, wajibu wangu" kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Bahi Sokoni katika Halmashauri ya Bahi wenye Lengo la  kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili. 

"Bodaboda tuendelee kufuata maelekezo ambayo tunapewa juu ya umuhimu wa sisi kuchukua tahadhari ili kuongeza usalama wetu kwa kuangalia abiria tunao wapakia. Kama unaona humuelewi, achana naye usimpakie ili kuondoka na adha za namna hii" Ameagiza Mhe. Senyamule 

Kero hiyo, iliibuliwa na mmoja wa wakazi wa eneo hilo Bw. Andrew Laurent wakati wa mkutano huo ambapo amesema siku za hivi karibuni kumetokea matukio ya aina hiyo ambayo yamekuwa kero kwa Maafisa usafirishaji hao hivyo kuhatarisha usalama wao. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Gift Msuya pamoja na kueleza mkakati wa Wilaya kukabiliana na uhalifu huo, amewasihi wananchi hususani Maafisa usafirishaji hao kushikamana kukabiliana na tatizo hilo. 

Awali kabla ya Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa alishiriki kikao cha  Baraza la Madiwani kujadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa hesabu zilizoishia Juni 30, 2023. 

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayewakilisha Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Donald Mejitii ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata Hati Safi na kuwasihi kuendelea na mshikamano huo. 

Kadhalika Mhe. Senyamule, ameiagiza Wilaya ya Bahi kupeleka mapato ya ndani kiasi cha Shilingi shilingi Milioni 223 kwenye Miradi ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye ripoti ya CAG.

$$$

#keroyakowajibuwangu
#dodomafahariyawatanzania

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA