VYOMBO VYA USALAMA VYAAGIZWA KUCHUKUA HATUA VITENDO VYA KIKATILI KWA WATOTO







Agizo limetolewa kwa vyombo vya usalama Mkoa wa Dodoma kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vya kikatili vilivyoibuka hivi karibuni kwa watoto ikiwemo mauaji na kukatwa baadhi ya viungo vya mwili katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule ametoa agizo hilo wakati wa mkutano wa hadhara alioufanya na wananchi wa Kata ya Ipagala kwenye ofisi za Kata hiyo Jijini Dodoma Julai 22, 2024 wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili.

“Jambo la Mtoto kutekwa halivumiliki na Serikali. Matukio haya yanafahamika na yanafanyiwa kazi na yeyote atakayebainika kuhusika, atachukuliwa hatua za kisheria. Natoa agizo kwa vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka kwa matukio yanayosababisha vifo ili jambo hili lifike mwisho” RC Senyamule.

Aidha, agizo hilo limefuatia kero iliyowasilishwa mbele ya Mkuu wa Mkoa huyo na moja kati ya wakazi wa eneo hilo aliyelalamikia uwepo wa matukio hayo kwenye eneo lao sambamba na kuiomba Serikali ijenge kituo cha Polisi kwenye Kata hiyo.

Akitoa jawabu la kero hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Theopista Mallya, amesema tayari Serikali imetangaza ujenzi wa vituo vya Polisi kwenye kila Kata japo kuwa kama jamii inauhitaji wa haraka inashauriwa kujenga kwa nguvu zao boma la kituo na Serikali itamalizia.

Mkutano huo uliibua kero mbalimbali zikiwemo ardhi na maji na zote zilipatiwa majawabu ambapo Mkurugenzi wa Jiji atafungua kliniki fupi ya ardhi Julai 24 katika eneo hilo huku DUWASA wakitarajia kutekeleza mradi wa shilingi Bilioni 10.2 utakaotatua kero ya maji safi na mradi wa uboreshaji maji taka kwa gharama ya shilingi Bilioni 164.

 #dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu

 

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA