RC ARIDHISHWA UTEKELEZWAJI WA MIRADI, ALIPONGEZA JIJI LA DODOMA.
Septemba 11, 2024
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametembelea na kukagua miradi ya
Elimu na Afya inayotekelezwa katika kata nne (4) ambazo ni kata ya Zuzu, Nala,
Kikuyu kaskazini na Tambukareli zinazopatikana katika Halmashauri ya Jiji la
Dodoma.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa ziara hiyo RC Senyamule
amewataka uongozi wa Jiji la Dodoma
kukamilisha miradi kwa wakati hususan miradi iliyotakiwa kukamilika katika
kipindi cha mwaka wa fedha uliomalizika wa 2023/ 24 na kuwataka kukamilisha miradi
hiyo Ifikapo Mwishoni mwa mwaka huu na wananchi waanze kupatiwa huduma.
‘’Mnapopata fedha za miradi mnatakiwa mzitoe mapema ili kuikamilisha
miradi kwa wakati kwasababu kumekuwa na uchelewaji wa kutekeleza miradi
kunakotokana na mwaka wa fedha kumalizika, hivyo nitoe wito kwa Jiji kuhakikisha
miradi yote inakamilika na inaanza kutoa huduma kwa wananchi kwa muda
uliokusudiwa.
Awali akizungumza katika mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya
Zuzu kinachotarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, 2024 Senyamule ametoa maagizo kwa Halmashauri zote
za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanaanza mapema maandalizi ya kutumika kwa vituo
vya afya kwa kufanya maandalizi yote Muhimu yanayohitajika.
‘’Tunafahamu tupo katika kampeni ya kupunguza vifo vya mama
na mtoto na ujenzi wa vituo vya afya hivi ni katika kuweka huduma za afya
karibu na wananchi ili kuepusha vifo vinavyoepukika vinavyotokana na umbali wa
huduma hizo, nitoe maagizo kwa Halmashauri zote kuhakikisha wakati
wanakamilisha ujenzi wa vituo vya afya pia endeleeni na mchakato wa kuanza manunuzi
ya vifaa tiba na watoa huduma katika vituo hivyo ili vitakapokamilika tuu
vianze kutoa huduma Mara moja’’.
Katika kuhakikisha na kuweka mazingira bora na ya kuvutia
katika vituo vya afya na Hospitali za Mkoa wa Dodoma Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa
Dkt. Nassoro Matuzya, amemuagiza Mganga Mkuu wa Jiji hilo pamoja na watumishi
wote wa ofisi yake kupanda miti mine (4) kila mmoja na kuisimamia hadi itakapokua
katika mradi wa Hospitali ya Wilaya hiyo inayojengwa katika kata ya Nala.
Hatahivyo Mhe.
Senyamule amewapongeza Jiji hilo kwa Usimamizi mzuri wa miradi pamoja
kutekeleza miradi mbalimbali kupitia mapato ya ndani ikiwa ni sehemu ya
kurudisha kwa kwa jamii (SCR) hali inayochangia mahusiano mazuri kwa Jamii
inayowazunguka.
Katika ziara hiyo amekagua ujenzi wa miradi ya Kituo cha
Afya Zuzu unaogharimu Tsh. 259,000,000, Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma
Unaogharimu Tsh. Billioni 1.5, Ujenzi wa Vyumba 2 vya madarasa na Matundu 8 ya
vyoo katika Shule za Sekondari Kikuyu na Sechelela Unaogharimu Milioni Tsh 120,800,000
@ 60,400,000 ambapo ujenzi wa Miradi yote upo katika hatua ya Umaliziaji.
Comments
Post a Comment