KAMPUNI YA OFFGRIDSUN YATAMBULISHA MRADI WA MAJIKO SANIFU NA BANIFU DODOMA
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, leo Oktoba 29, 2024, ametembelewa na ugeni kutoka Kampuni ya OFFGRIDSUN ya nchini Italia katika ofisi yake iliyopo katika jengo la Mkapa Jijini Dodoma.
Kampuni hiyo inayojishughulisha na usambazaji wa nishati jua (solar enegy) kwenye nchi za Kenya, Rwanda, Angola na Tanzania, kwa sasa imekuja na mradi mwingine mpya wa ‘Green Cook stove’ utengenezaji na usambazaji wa majiko sanifu na banifu yanayotumia nishati safi.
Lengo la kumtembelea Mkuu wa Mkoa ni kutambulisha mradi huo unaotekelezwa kwenye mikoa mitatu hapa nchini ambayo ni Dodoma, Morogoro na Tanga. Mkoani hapa, mradi unatekelezwa kwenye Halmashauri mbili za Chamwino na Kongwa ambapo lengo ni kuzifikia kaya 23,000 za Chamwino na 26,000 za Kongwa.
Akitoa ufafanuzi juu ya lengo la mradi huo hapa Dodoma, mwakilishi wa Kampuni hiyo nchini Bi. Valentina Quaranta, amesema;
“Mradi unalenga kusambaza majiko sanifu yatakayopunguza uzalishaji wa hewaukaa kwa asilimia 50. Katika kipindi cha miaka miwili, tunatarajia kusambaza majiko 200,000 ambapo kwa kuanza, kwa mwaka mmoja tutazalisha majiko 20,000 na kila mwaka tutaweza kuzalisha majiko 40,000”. Bi. Quaranta
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameishukuru Kampuni hiyo kwa kutumia fursa na kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye matumizi ya nishati safi na kuongeza kuwa Serikali ipo kwenye mkakati wa kupunguza gharama za nishati ya gesi ili wananchi wote waweze kutumia.
“Ili mradi wenu uweze kuwafikia wanufaika wengi zaidi hasa maeneo hayo ya vijijini, ni vyema mkatoa majiko hayo bila gharama kwani Serikali kwa sasa ipo kwenye mkakati wa kupunguza gharama za gesi kwa kiasi kikubwa ili wananchji wake waweze kuitumia kupikia ili kufikia mwaka 2030, asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi” Mhe. Senyamule.
Kampuni ya OFFGRIDSUN ilianza kufanya kazi mwaka 2022 na kuanza ushirikiano na Tanzania mwaka 2023. Ilianza kwa kutengeneza na kusambaza bidhaa zinazotumia nishati ya jua lakini kwa sasa inatengeneza na kusambaza majiko yanayotumia nishati safi yenye kiwanda chake Jijini Dar Es Salaam.
#kurayakosautiyako
#ujanjanikupigakura
#dodomatukotayarikupigakura
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment