RAS DODOMA ATEMBELEA MRADI WA JP-RWEE UNAOTEKELEZWA CHAMWINO













Na. Hellen M. Minja,           
       Habari – DODOMA RS

Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar K. Mmuya, ametembelea vikundi vya kina mama wajasiriamali wadogo pamoja na wakulima wanaowezeshwa na mashirika ya kimataifa kulima na kutengeneza bidhaa kitaalamu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Oktoba 29,2024.

Vikundi hivyo kutoka katika vijiji vya Chamwino Ikulu, Nayu na Dabalo vipo chini ya mradi unaojulikana kama JP-RWEE unaofadhiliwa na mashirika manne ya kimataifa ambayo ni FAO, IFAD, WFP na UN-WOMEN wenye lengo la kuboresha maisha ya wanawake waishio vijijini.

Akiongea na wanawake walio kwenye mradi wa kuwezeshwa kupata hati miliki za ardhi katika kijiji cha Nayu, Kata ya Badalo, Bw. Mmuya ametoa wito kwa mashirika hayo kuwashirikisha wanawake hao kwenye kila wanachokifanya ili waweze kuwa na uelewa wa kutosha.

“Shughuli zote za Serikali tunazozifanya, tuwaunganishe wananchi na Serikali yao wajue nini Serikali inawafanyia. Hiki ninachokieleza ni mpango wa Serikali kuwawezesha wananchi wake kumiliki ardhi kisheria, hiyo inatusaidia sisi kupunguza migogoro ya ardhi lakini pia kupunguza unyanyasaji wa kijinsia” Bw. Mmuya.

Aidha, akiwasilisha moja ya matokeo tarajiwa ya mradi kwa niaba ya Katibu Tawala Wilaya ya Chamwino, Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo Bw. Living Kilawe, amesema, wanatarajia kuongezeka kwa upatikanaji wa rasilimali, mali na teknolojia muhimu kwa uzalishaji wa kilimo unaostahimili hali ya hewa na usalama wa chakula na lishe.

Kadhalika, Mratibu wa Mradi kutoka WFP Bw. Abiudi Gamba, amesema mradi wa JP-RWEE unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, umeanza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika 2027 ukihamasisha kilimo cha mazao ya Mtama, mboga mboga na Alizeti lakini zaidi ya hayo kuna shughuli za kiuchumi zinazofanyika.

Mradi wa JP-RWEE unatekelezwa katika Kata 18 na Vijiji 40 ukilenga jumla ya wanawake 8,000. 3,500 kutoka Mkoa wa Singida (Ikungi), 3,500 kutoka Dodoma (Chamwino) na 1,000 kutoka Zanzibar ili kuhakikisha haki na ustawi wa wanawake unafikiwa kuelekea Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu.

 

#kurayakosautiyako               
#ujanjanikupigakura               
#dodomatukotayarikupigakura
#mtiwangubirthdayyangu















 

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA