RC SENYAMULE ATATUA MGOGORO WA UJENZI WA SHULE KIDOKA - CHEMBA









Na. Hellen M. Minja,         
       Habari – DODOMA RS

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule, leo Oktoba 31, 2024, ametatua mgogoro kati ya wananchi wa Kata ya Kidoka juu ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kata, kufuatia Wananchi wa  vijiji viwili vya Kidoka na Pangalua  vilivyoko katika kata ya Kidoka,Halmashauri ya wilaya ya Chemba, wote kutaka   shule ijengwe kwenye vijiji vyao.

Mkuu wa Mkoa huyo ametatua mgogoro huo wakati wa mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Pangalua,mkutano ambao lengo lake ni  kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wakazi wa kata hiyo,ikiwemo eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kata.

“Serikali imeona wote mna mahitaji ya shule, mabishano haya yanatokana na dhamira njema, japo inatuchelewesha kwani ilitakiwa kufanyiwa maamuzi ya haraka. Tumeamua shule zijengwe mbili, kwa maana ya Kidoka na Pangalua. Shule mbili zitajengwa, kila Kijiji  kipate ya kwake” Amesema Mhe. Senyamule.

Baada ya uamuzi huo, Mkuu wa Mkoa amesema fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule moja, sasa zitagawanywa kwa ujenzi wa shule mbili na kuwaasa wazazi kupeleka watoto wao shule.

“Hizo fedha zitagawanywa mara mbili, Kidoka itakwenda shilingi 249,763,750 na Pangalua itakuja shilingi 294,461,876. Nimesikitika kwa kuwa leo nilijipanga kuja kuanza ujenzi maana tumechelewa miezi minne nyuma, tuna miezi miwili tu kukamilisha haya majengo ili mwezi wa kwanza, watoto wetu waanze shule”. RC Senyamule

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Halima Okash, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kumaliza mgogoro huo kwani wananchi wa Kata hiyo sasa watakua na amani.

“Hapa najua wanachi hawa wakiondoka, nafsi zao zitakua zimetulia sana kwa sababu mgogoro huu wa ujenzi wa shule umetatatuliwa. Mhe. Mkuu wa Mkoa tunakushukuru sana. Sisi kama Serikali katika ngazi hii ya Wilaya, Tarafa, Kata pamoja na Kijiji,tumepokea maelekezo yako na tupo tayari kuyatekeleza” DC Okash.

 

#kurayakosautiyako               
#ujanjanikupigakura               
#dodomatukotayarikupigakura
#mtiwangubirthdayyangu








 

Comments

Popular posts from this blog

WALIMU WATAKIWA KUFUNDISHA UZALENDO SHULENI.

TRAMPA KANDA YA KATI WAFANYA KIKAO DODOMA

BARAZA LA MITUME NA MANABII WAMTEMBELEA MKUU WA MKOA WA DODOMA