MWAMKO WA WANAWAKE KUGOMBEA SERIKALI ZA MITAA WAONEKANA DODOMA
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Wanawake wametajwa kuonesha mwamko mkubwa kwa kujitokeza kugombea nafasi za wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa pamoja na wajumbe wa Halmashauri za Vijiji /wajumbe wa kamati za mitaa ambapo wanawake 260 wamejitokeza kugombea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 Mkoa wa Dodoma.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipokua akizungumza na waandishi wa Habari leo Novemba 26, 2024 katika ukumbi wa Ofisi yake, Jengo la Mkapa Jijini Dodoma kuutangazia Umma juu ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika kesho Novemba 27, 2024.
“Katika ngazi ya Mitaa na Vijiji, wanawake 53 wamejitokeza kugombea nafasi za wenyeviti lakini katika ngazi ya vitongoji, wanawake 207 wamejitokeza kugombea nafasi hizo. Hii ni kuonesha kuwa angalau kumekua na mwamko sasa wa usawa wa kijinsia katika maeneo yetu”. Amesema Mhe. Senyamule.
Aidha, ametaja baadhi ya majukumu ya wenyeviti wa Serikali za mitaa kuwa ni pamoja na kutunza rejesta ya wakazi wa maeneo yao na nyaraka nyingine muhimu zinazohusu maendeleo ya maeneo yao pamoja na kumbukumbu za vizazi na vifo, kusimamia ulinzi na usalama wa watu na mali zao pamoja na nyingine nyingi..
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa, ametoa shime kwa wananchi wa Mkoa wake kujitokea kwa wingi kutimiza haki yao ya Kidemokrasia kwa kuchagua viongozi watakaowafaa.
“Nitoe shime kwa Wanadodoma wote, wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili kuhakikisha sauti zao zinasikika na kwamba wanaweza kuchagua Viongozi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao kwani vituo vya kupigia kura ni vya kutosha kwa ujumla wake ni 4,011” Mhe. Senyamule
Kadhalika, ametoa shukrani kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha demokrasia ya Nchi yetu kwa vitendo, na kutangaza siku ya tarehe 27/11/2024 kuwa siku ya mapumziko, ili Watanzania wapate nafasi ya kushiriki fursa hii adhimu ya kupiga kura.
“Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi”
#kurayakosautiyako
#ujanjanikupigakura
#dodomatukotayarikupigakura
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment