RC SENYAMULE AHIMIZA WANADODOMA KUJITOKEZA KUPIGA KURA
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Wito umetolewa kwa Wakaazi wa Mkoa wa Dodoma kufika katika vituo walivyojiandikishia kwa ajili ya kutimiza haki ya kidemokrasia kwa kushiriki kupiga kura kuchagua Viongozi wa Serikali za Mitaa yao pamoja na kulinda amani.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule aliposhiriki zoezi hilo katika kituo chake alichojiandikishia Shule ya Msingi Dodoma Mlimani, Mtaa wa Salmini, Kata ya Tambukareli Jijini Dodoma mapema leo Novemba 27, 2024.
“Siku ya leo ni ya muhimu sana Dodoma kuwa salama. Tukumbuke kauli yetu ‘Uchaguzi salama kwa maendeleo ya Taifa letu’. Nitoe wito kuwa asikose mtu kwenda kupiga kura kwenye kituo alichojiandikishia na kila mmoja ahakikishe analinda usalama” Amesisitiza Mhe. Senyamule
Kadhalika, amewashukuru wana Dodoma wote kwa kuendelea kutunza amani na utulivu wakati wote tangu kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi, wakati wa kampeni hadi leo hii unapokwenda kutamatika.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar K. Mmuya, amepiga kura katika kituo alichojiandikishia Mtaa wa Mathias, Kata ya Miyuji, Jijini Dodoma na kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwani vituo vipo karibu na makaazi ili kutimiza haki ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Miongoni mwa viongozi wastaafu wa Mkoa wa Dodoma aliyepata nafasi ya kushiriki zoezi hilo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ni Bw. Peter Mavunde (Meya mstaafu wa Jiji la Dodoma) ambapo ametoa hamasa kwa wanachi kujitokeza mapema, kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura ili kutimiza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi watakaowafaa.
“Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi”
#kurayakosautiyako
#ujanjanikupigakura
#dodomatukotayarikupigakura
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment