Yas YATAMBULISHA HUDUMA ZAKE MKOA WA DODOMA
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Uongozi wa Kampuni ya mawasiliano nchini, @Yas umemtembea Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar Mmuya ofisini kwake jengo la Mkapa Jijini Dodoma leo Novemba 28, 2024 kwa lengo la kutambulisha mabadiliko yaliyotokea kwenye kampuni hiyo ambayo awali ilijulikana kama Tigo pamoja na huduma zake.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, amewashukuru kwa kufika kutambulisha mabadiliko hayo kwa Uongozi wa Mkoa na kuwataka kushirikiana kwa kila fursa itakayoonekana.
“Nawashukuru na ninawapongeza kwa mabadiliko yanayoonekana kwenye mawasiliano na watumiaji wamekubali mabadiliko hayo. Teknolojia ina harakisha maendeleo hivyo, kama kuna fursa yeyote hapa Mkoani mniambie kwa kuwa lengo ni kujenga huu Mkoa, ichukulieni Dodoma tofauti na muwe na mkakati maalum kwa ajili ya Dodoma” Amesema Bw. Mmuya.
Kadhalika, Mkurugenzi wa Kanda ya kati wa Kampuni hiyo Bw. Said Idd amesema kampuni hiyo imefanya mabadiliko kwa lengo la kuboresha huduma kwa ubora zaidi kwani mpaka sasa wameweza kuwafikia Watanzania Nchi nzima kwa mtandao wenye kiwango cha 4G na 5G.
Aidha,Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa ;
"Tumebadilisha chapa yetu ili kuendana na maono yetu ya baadaye na kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu. Chapa yetu mpya ina akisi dhamira yetu ya kuendeleza ubunifu, huduma bora kwa kuzingatia mahitaji ya wateja wetu wa Kanda ya Kati na Nchi nzima kwa Ujumla."
Uongozi wa kampuni hiyo uliomtembelea Katibu Tawala Mkoa ni pamoja na Bw. Richard Mmari - Meneja Kanda ya kati, Tinna Mrisho - Meneja Masoko Kanda ya kati,Frank Anthony na Martin Mavura ambao ni Mameneja mauzo Dodoma.
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment