DODOMA NA MIKAKATI MADHUBUTI YA KUKUZA UCHUMI.
Mkuu wa MKoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule akizungumzia namna Mkoa wa Dodoma unavyokua kwa kasi kiuchumi katika kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Dodoma kilichofanyika jana katika ukumbi wa Hoteli ya Vizano Jijini Dodoma.
Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia akitaja vitengeneza fursa ambavyo vinapaswa kutumika ipasavyo ili kukuza uchumi kuwa ni Malikale wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Dodoma kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Vizano Jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (katikati) akimkabidhi cheti Balozi wa Mkoa wa Dodoma nchini China Bw. Japhet Konzo mara baada ya kufunga kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Dodoma
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Dodoma wakifuatilia kwa makini mawasilisho mbalimbali wakati kikao hicho kikiendelea hapo jana katika ukumbi wa Hoteli ya Vizano Jijini Dodoma
Na. Sizah Kangalawe Habari- Dodoma Rs
Uchumi wa Wananchi wa Mkoa wa Dodoma unaendelea kukua siku hadi siku kutokana na uwepo wa ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita Mkoani hapa, hali inayosababisha Jiji la Dodoma kukua kwa kasi.
Ni katika kikao kazi cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dodoma (RCC), ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ameweka bayana ukuaji wa Mji huu unaotokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuhamia kwa Makao Makuu ya Serikali na Ujenzi wa miradi mikubwa kama Uwanja wa Ndege Msalato na treni ya mwendokasi (SGR).
Kikao kazi hicho kimefanyika Desemba 19, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Vizano hoteli Jijini Dodoma.
"Mimi nikitembea Dodoma kila siku nakuta miji mipya imeanzishwa na Wananchi, wengine wanahitaji barabara na maji, hii inaonesha kuwa Mji wa Dodoma unakua kwa kasi.Bado tunajivunia miradi ambayo imetumia Fedha nyingi sana za Serikali, lengo kuu la miradi hii ni kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Dodoma, lakini pia uchumi wa Serikali yetu.
Sisi Mkoa tunatakiwa tufikiri tunakwenda kufanya nini ili tuone tunaongezaje kipato cha mtu mmojammoja kupitia miradi hii mikubwa ambayo Mhe.Rais wetu amewekeza fedha nyingi katika miundombinu, sisi tunaongezaje kipato cha Taifa kupitia miundombinu hii ? yaani tunaweza kupata faida gani kupitia miradi hii", amebainisha Mhe. Senyamule
Aidha Mhe. Senyamule amezitaka Halmashauri zote za Dodoma zitafute njia mbalimbali za kukuza uchumi, huku akiwasihi Wanadodoma mmoja mmoja kujishughulisha katika kazi mbalimbali zitakazowasaidia kujipatia kipato na kukuza uchumi wao,kadhalika uchumi wa Mkoa.
Naye Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia amevitaja vitengeneza fursa ambavyo vinapaswa kutumika ipasavyo ili kukuza uchumi kuwa ni Malikale, Mkao wa kijiografia, jua na upepo, hali ya hewa, madini, maji, ardhi, Makao Makuu ya Serikali, uongozi bora, miundombinu wezeshi na uwepo wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Utafiti, miundombinu saidizi ( masoko, minada na majengo ya biashara nk).
Katika hatua nyingine, Mhe. Senyamule ametumia kikao hicho kumkabidhi barua ya kumtambulisha Bw.Japhet P. Konzo, Mtanzania anayeishi Nchini China kuwa Balozi wa Dodoma Nchini humo ambaye atautangaza Mkoa na fursa zote zinazopatikana.
Akizungumza baada ya utambulisho huo amesema" nichukue nafasi hii kumshukuru Mkuu wa Mkoa na Serikali ya Mkoa wa Dodoma kwa kunipa nafasi ya kuwa Balozi wa Mkoa Nchini China, nchi ambayo imeendelea sana kwenye masuala ya teknolojia.
Mimi kama Balozi nitajitahidi kuona ni kwa jinsi gani naweza kuleta teknolojia hizo katika Mkoa wetu ili tuhakikishe kwamba tunaongeza tija kwenye masuala ya kilimo kwa kutumia teknolojia", amesema Bw. Konzo
Kikao kazi hicho kimefanyika Mwenyekiti akiwa ni Mkuu wa Mkoa, na wajumbe ni Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakuu wa taasisi zilizopo ndani ya Mkoa, Wabunge na Wadau mbalimbali wa Maendeleo.
Comments
Post a Comment