MTI WANGU BIRTHDAY YANGU DESEMBA, YAPANDA MITI 400 JK SQURE
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar Mmuya akizungumza wakati wa hafla ya kupanda miti 'Team December' kuendeleza kampeni ya 'mti wangu birthday yangu' katika viwanja vya JK Square UDOM Jijini Dodoma Kampeni iliyozinduliwa rasmi Oktoba 18, 2024 katika Chuo hicho.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Jeshi la Uhifadhi, Mkuu wa Ofisi ya Mahusiano TANAPA Dodoma Dkt. Noelia A. Myonga akielezea namna alivyofarijika na zoezi la kukijanisha Dodoma katika eneo la JK Square kwani linakumbusha uumbaji wa Mungu
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Winiesta Saria akizungumza na hadhira iliyoshiriki kampeni ya mti wangu birthday yangu katika eneo la JK Squre ndani ya Chuo Kikuu cha Dodoma na kusema kuwa kupanda miti ni ajenda ya Chuo hicho.
Mmoja kati ya wazaliwa wa mwezi Disemba akipanda mti wakati wa Kampeni ya mti wangu birthday yangu ambayo hufanyika kila tarehe 18 ya mwezi ambapo mwezi huu iliendelea kufanyika katika eneo la JK Square (UDOM) ambapo miti 400 ilipandwa.
Baadhi ya wazaliwa wa mwezi Disemba wakiongozwa na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Kaspar Mmuya kukata keki kama ishara ya kumbukizi ya siku zao za kuzaliwa baada ya kupanda miti katika eneo la JK Squre (UDOM) jana Disemba 18, 2024.
Wageni waalikwa, watumishi kutoka Taasisi mbalimbali za Mkoa wa Dodoma na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na Chuo KIkuu cha Dodoma waliohudhuria hafla ya upandaji miti kama kumbukizi ya siku za kuzaliwa mwezi Disemba
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Kampeni ya Mti,Wangu Birthday Yangu inayoendeshwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, kwa mara nyingine imefanikiwa kuwakutanisha baadhi ya Wakazi wa Mkoa wa Dodoma, Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na baadhi ya Watumishi wa Taasisi za Serikali zilizopo katika mkoa huu kama TFS,TANESCO,TANROADS, TANAPA na TARURA waliozaliwa mwezi wa 12, maarufu kama 'Team December ' kupanda miti hapo jana Desemba 18, 2024, huku wakisindikizwa na watumishi wenzao kutoka kwenye Taasisi hizo,ambapo kwa umoja wao walifanikiwa kupanda miti 400 pembezoni mwa barabara ya kuzunguka eneo la JK. Squre lililopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kupendezesha mandhari yake kwani linatarajiwa kuwa eneo la kupumzikia na kufanyia hafla mbalimbali.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo inayofanyika kila mwezi, Muasisi wa Kampeni hiyo inayounga mkono kampeni mama ya ‘Kijanisha Dodoma’ Katibu Tawala Mkoa Bw. Kaspar K. Mmuya amesema;
“Leo hii tumepanda miti 400 na miti ile tumepanda kimkakati, pembezoni mwa barabara, na itakua kama kiashiria kwamba huku kuna kitu hivyo ukuaji wake utakuwa na ukomo ili kupendezesha hili eneo. Tunataka hapo baadae litumike kwa shughuli mbalimbali bila kuweka mahema kwani kutakua na kivuli cha kutosha.” Bw. Mmuya.
Kamishna Mwandamizi Msaidizi na Meneja wa rasilimali za nyuki kutoka Wakala wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TFS) Bw. Hussein Msuya, amesema miti ni uhai kwani hewa ya oksijeni tunayoitumia inatoka kwenye miti, pia ni rasilimali kwa ajili ya nyuki ambao wanatumia maua kuzalisha asali hivyo ukiondoa miti, umeondoa nyuki duniani.
Aidha,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Jeshi la Uhifadhi, Mkuu wa Ofisi ya Mahusiano TANAPA Dodoma Dkt. Noelia A. Myonga amesema amefarijika na zoezi la kukijanisha Dodoma kwani linakumbusha uumbaji wa Mungu ambaye aliumba mazingira yote kisha mwanadamu ili aweze kuyasimamia na kuyatunza mazingira hayo.
Naye, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Profesa Winiesta Saria alisema kupanda miti ni ajenda ya Chuo hicho, na siku ya Jumamosi Desemba 14, 2024 walipanda miti 6,500 lengo likiwa ni kukizungushia chuo uzio wa miti ili isaidie mipaka, matunda pamoja na kuongeza kiwango cha mvua kwa siku za usoni,kwani kwa sasa mvua zinanyesha Dodoma kwa siku 35 tu kwa mwaka hivyo kupanda miti kutasababisha mvua kuongezeka.
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment