RC SENYAMULE NA STAMICO WASHIRIKI CHAKULA CHA PAMOJA SAMARIA - HOMBOLO
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, akizungumza na wazee wa kijiji cha Samiria aliposhiriki chakula cha pamoja na kundi hilo la wazee wenye ugonjwa wa ukoma wanaoishi katika Kata ya Hombolo Bwawani, Jijini Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akimlisha keki Mmoja wa wazee wa Kijiji cha Samaria alipofika kushiriki chakula cha pamoja na kuwashika mkono kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka
Baadhi ya wana kikundi cha Wanawake na Samia cha Mkoa wa Dodoma wakigawa chakula kwa watoto wa kijiji cha Samaria wakati wa hafla ya kuwashika mkono wazee wa kijiji hicho kwa kutoa misaada na kushiriki chakula cha pamoja
Baadhi ya Wazee wa kijiji cha Samaria kilichopo Hombolo Jijini Dodoma wakipiga makofi wakati wa hafla ya chakula cha pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Senyamule na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Disemba 23, 2024
Baadhi ya Wazee wa Samaria (picha juu na chini) wakipokea misaada iliyopelekwa kijijini hapo na STAMICO kwa ajili ya kuwashika mkono kwa mahitaji muhimu baada ya kushiriki chakula cha pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO na Kikundi cha wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, Disemba 23, 2024, alipata fursa ya kushiriki chakula cha pamoja na kundi la wazee wenye ugonjwa wa ukoma wanaoishi katika eneo la Samaria katika Mtaa wa Kolimba, Kata ya Hombolo Bwawani, Jijini Dodoma
Chakula hicho cha pamoja kilichoambatana na ugawaji wa mahitaji mbalimbali ya muhimu, kiliandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake kwa kushirikiana na kikundi cha Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma ambao kwa pamoja wamejitolea kuwa walezi wa wazee.
Akizungumza na wazee hao, Mhe. Senyamule amesema kuwa kundi hilo ni la muhimu katika jamii kama walivyo watu wengine hivyo jamii inapaswa kulipa thamani na kushirikiana nalo katika shughuli nyanja zote stahiki.
“Leo tumekuja kula na nyinyi na kuwaonesha hii Tanzania ni ya kwenu sote na nyinyi na sisi ni watu tunaofanana kwa maana ya mahitaji ya kibinadamu. Nyinyi ni watu wa thamani na pekee. Mhe. Rais anatamani watu wote wapate haki sawa kama binadamu, waishi kwa furaha na amani” Amesema Mhe. Senyamule.
Aidha, Mhe. Senyamule ameagiza kitengo cha Ustawi wa Jamii kuandaa programu kwa wanasamaria kupatiwa elimu ya uzalishaji na ujasiriamali ili waweze kujikwamua bila kutegemea misaada kwani Mhe. Rais ameanzisha programu nyingi za kusaidia makundi maalum.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwase, aliongelea umuhimu wa jukumu la kusaidia wenye mahitaji ili kuleta usawa katika jamii.
“Aliyetuumba hakuchagua kupeleka wengine wakateseka na wengine wakafurahie, dhumuni la Mungu lilikua tuwe na fursa sawa lakini mwisho wake tuwe na furaha na amani. Sisi tuna wajibu wa kuwaangalia wale ambao wapo kwenye changamoto angalau waje kwenye furaha na amani.
Naye, Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma Bi. Fatma Madidi alieleza namna alivyolifahamu eneo hilo na kugundua uwepo wa wahitaji kwani walipofika hapo walikuta hali ya maisha sio ya kuridhisha hivyo walishirikisha Serikali ya Mkoa na Shirika la STAMICO na kuandaa utaratibu wa kuwashika mkono wazee hao hasa kwa kutoa mahitaji ya chakula, vifaa tiba na dawa.
Kijiji cha Samaria linakaliwa na wakazi takribani 180 likiwa na Kaya 23 ambazo zinaishi kwa kutegemea misaada kutoka kwa wahisani kutokana na kukosa nguvu kazi ya kutosha kutokana na ulemavu walionao uliotokana na ugojwa wa ukoma hivyo, tangu kujitokeza kwa STAMICO, limekua msaada kwao kwa mahitaji muhimu.
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment