MKOA WA DODOMA WAENDELEA NA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KIFUA KIKUU
Mratibu wa Huduma za kudhibiti Kifua Kikuu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Allan Tarimo, akizungumzia malengo matatu ya Mpango wa kuibua wagonjwa wenye vimelea vya Kifua Kikuu wakati wa Kikao kazi cha vituo vya huduma za Afya binafsi vinavyotoa huduma za ugonjwa huo pamoja na wadau kilichofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa Jijini humu leo Januari 31, 2025
Mratibu wa Kifua Kikuu na ukoma Mkoa wa Dodoma Dkt. Peres Lukango (aliyesimama) akielezea hali ya utoaji huduma za Kifua Kikuu wakati wa Kikao kazi cha vituo vya huduma za Afya binafsi vinavyotoa huduma za ugonjwa huo pamoja na wadau kilichofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa Jijini humu leo Januari 31, 2025
Picha juu na chini, baadhi ya watoa huduma kutoka vituo binafsi vya huduma za afya hususan Kifua Kikuu na wadau mbalimbali wakifuatilia Kikao kazi kilicholenga kufanya tathmini ya uibuaji wa wagonjwa wenye vimelea vya ugonjwa huo kilichofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa Jijini humu leo Januari 31, 2025
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Kufuatia changamoto ya uibuaji Wagonjwa wa Kifua Kikuu kuelekea kwenye lengo la Dunia la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030, Seksheni ya Afya Mkoa wa Dodoma chini ya Wizara ya Afya, leo Januari 31, 2025, wamefanya kikao kazi cha kujadili namna ya kufikia lengo la uibuaji wagonjwa kwa kushirikiana na vituo binafsi vya afya na Wadau.
Akizungumza na wadau hao katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma jengo la Mkapa Jijini Dodoma, Mganga Mkuu wa Mkoa Dr. Thomas Rutachunzibwa, ameelezea umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na vituo binafsi ili kufikia malengo lakini pia ametoa angalizo juu ya utoaji ‘takwimu hewa’ za wagonjwa wa Kifua Kikuu.
“Niombe wenzetu wa vituo binafsi, tusaidiane kuwahudumia wananchi tuhakikishe kwamba lengo tulilopewa tunalifikia ikiwezekana na kulizidisha sio tunafikia hilo lengo na kusema tumemaliza, haya malengo ni makisio tu, kama umepewa wagonjwa 10 lakini uhalisia kuna wagonjwa 20, waibue wote.
“Tusije tukaleta takwimu hewa, ukisema nimeibua 10 kumbe humo kuna watatu ambao sio wagonjwa, tutakwenda kuaibika huko mbele. Naomba turipoti wagonjwa wa kweli na tujitahidi kadri tunavyoibua kwa siku, takwimu zinaingizwa kwenye mfumo. Baadhi ya Halmashauri wamekua wakifanya kazi nzuri lakini ukija kwenye mfumo, hakuna taarifa,” Dr. Rutachunzibwa.
Akielezea malengo ya Mpango huo, Mratibu wa Huduma za kudhibiti Kifua Kikuu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Allan Tarimo, amesema Mpango huo una malengo makubwa matatu ambayo ni kupunguza vifo kwa 75% ikilinganishwa na mwaka 2015, kupunguza maambukizi kwa 50% na kupunguza changamoto za kiuchumi kwa mgojwa kwa 50%.
Kadhalika, Mratibu wa Kifua Kikuu na ukoma Mkoa wa Dodoma Dkt. Peres Lukango amesema, huduma za Kifua Kikuu zimejengwa kwenye utashi binafsi, hali inayosababisha huduma kushuka pindi Mtaalamu anapoondoka kwenye kituo husika hivyo, inapaswa huduma hizo ziwe sehemu ya kituo kizima na si mtu binafsi ili kufikia malengo.
Hata hivyo, Mwakilishi kutoka Hospitali ya Mt. Gemma ya Jijini Dodoma ambayo ni moja ya vituo vinavyotoa huduma za Kifua kikuu Dkt. Theodora, amesema Hospitali yake imepewa lengo la kufikia wagonjwa 16 na mpaka sasa wameshafikia wagonjwa 11 hivyo wanatarajia kufikia malengo waliyowekewa na zaidi.
Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa Mikoa 9 iliyo kwenye Mpango Harakishi wa kuibua wagonjwa wenye vimelea vya Kifua Kikuu Mpango ambao ulizinduliwa rasmi Januari 06, 2025 katika Wilaya ya Chamwino Mkoa wa Dodoma na Waziri mwenye dhamana ya Afya Mhe. Jenista Mhagama.
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment