RC SENYAMULE ATOA MSAADA WA MABATI KWA WAHITAJI
Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, leo Januari 27, 2025, ametoa msaada wa mabati na fedha taslimu shilingi Milioni Moja kwa wakazi wawili wa Mkoa wake wenye mahitaji maalum ambao wote wamefanikiwa kujenga nyumba hadi hatua ya lenta lakini wameshindwa kupaua kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Akikabidhi msaada huo, kwenye viwanja vya ofisi yake Jengo la Mkapa Jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amesema Mkoa unayo sababu ya kuwasaidia kumalizia pale walipofikia kwani tayari wameonesha juhudi za kuanza ujenzi wa nyumba na kuongeza kuwa Mhe. Rais anajali makundi yote katika jamii.
“Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan anajali makundi yote, ya kina mama na watu wenye ulemavu, ni makundi ambayo Serikali inayapa uzito wa pekee ndio maana tuliposikia uhitaji huu, tukaona tunayo sababu ya kupokea maelekezo ya Mhe. Rais ya kutekeleza yale ambayo yeye anatamani kuyaona kuhakikisha makundi haya yanakaa mahali salama”
“Kupitia kuweka mabati kwenye nyumba zenu, naamini sasa mtakua salama. Niwaombe muende mkatumie mabati haya kwa lengo lililokusudiwa kama mlivyoomba. Wataalamu wa Ustawi wa jamii mpo hapa, mtakwenda kuwatembelea kuona kazi ambayo wameifanya kutokana na hiki kidogo walichokipata” Ameongeza Mhe. Senyamule
Kadhalika, Bw. Kombo Jumbe ambaye ni mnufaika mwenye ulemavu wa miguu, ameishukuru Serikali ya Mkoa kwa msaada na kuonesha kuwajali watu wa makundi maalumu kwani alianza kujenga nyumba lakini kutokana na changamoto aliyonayo, ameshindwa kumalizia kuezeka hivyo, msaada alioupata utamtosha kumalizia nyumba yake.
Nae Bi. Farida Saidi, Mkazi wa Mkonze Jijini Dodoma, ambaye pia ni mnufaika wa mabati kwa ajili ya kuezekea nyumba yake, ametoa shukrani zake kwa Serikali ya Mkoa kwa kuonesha kuguswa na kadhia anayoipata hasa kipindi cha mvua kwani alijenga nyumba lakini akakwama kuezeka hali iliyopelekea kuweka maturubai pekee.
#dodomafahariyawatanzania
#keroyakowajibuwangu
#mtiwangubirthdayyangu
Comments
Post a Comment